NA SILIVIA AMANDIUS
BUKOBA.
Watoto wenye mahitaji maalumu katika Manispaa ya Bukoba na wilaya ya Muleba mkoani Kagera wameendelea kunufaika na msaada wa vifaa vya elimu na afya uliotolewa na Benki ya NMB wenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 103.2, ikiwa ni juhudi za kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuwapa fursa sawa watoto hao.
Kwa mujibu wa taarifa ya ugawaji wa vifaa hivyo, shule ya msingi Maendeleo imepatiwa samani za walimu zikiwemo viti na meza 6 pamoja na madawati 50, shule ya msingi Nshambya imepata madawati 40 na shule ya Ibura B madawati 100. Aidha, shule ya msingi Mugeza Mseto imepatiwa viti vya magurudumu 30 kwa ajili ya wanafunzi wenye ulemavu, hatua inayotarajiwa kurahisisha mahudhurio na ushiriki wao darasani.
Shule za sekondari Bukara na Maruku zimepatiwa vitanda vya ghorofa 50 kila moja, huku shule ya msingi Iyamahoro ikipatiwa vitanda vya kawaida pamoja na magodoro 40. Pia shule za msingi Kanyigo, sekondari Omumwan na sekondari Mugeza zimepata mabati na vifaa vya ujenzi, wakati zahanati ya Buhangaza Muleba ikipokea mabati 156 na zahanati ya Magereza Muleba ikipewa samani mbalimbali kwa ajili ya kuboresha huduma za afya.
Akiwasilisha taarifa hiyo, Meneja wa NMB Kanda ya Ziwa Ndg.Faraja Ng’ingo amesema benki hiyo ina wateja zaidi ya milioni 8 na tangu mwaka 2021 imekuwa ikirejesha kwa jamii zaidi ya shilingi milioni 24 katika miradi ya maendeleo bara na visiwani. Amesema msaada huo unalenga kuwagusa zaidi watoto wenye ulemavu ili waweze kupata mazingira bora ya elimu na huduma stahiki.
Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Mheshimiwa Erasto Sima, aliyekuwa mgeni rasmi kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera, amesema vifaa hivyo vitasaidia kupunguza changamoto zinazowakabili watoto wenye ulemavu, ikiwemo kushindwa kuhudhuria masomo kutokana na ukosefu wa vifaa muhimu. Amewahimiza wadau wengine kuendelea kujitoa kusaidia kundi hilo, hata kwa kutumia fursa za sherehe binafsi kuwagusa watoto hao.
Kwa upande wake, Meya wa Manispaa ya Bukoba, Mheshimiwa Acton Rwankomezi, ameishukuru NMB kwa msaada huo akieleza kuwa bado kuna upungufu wa zaidi ya madawati 1,000 katika manispaa hiyo. Amesema msaada uliotolewa utasaidia kupunguza changamoto hiyo na kuimarisha mazingira ya ujifunzaji kwa wanafunzi. Nao walimu na walezi wa watoto wenye ulemavu wameishukuru NMB na kuitaka jamii kuendelea kushirikiana kuwasaidia watoto hao ili waweze kufikia ndoto zao.

