Na.Sophia Kingimali,Dar es salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, ametoa rai kwa madaktari nchini kutumia teknolojia za kisasa ikiwemo akili bandia (AI) katika kuboresha utoaji wa huduma za afya za kibingwa na ubingwa bobezi nchini.
Wito huo ameutoa leo Aprili 16,2026 Jijini Dar es salaam wakati akifungua rasmi Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Upasuaji wa Ubongo (Neurosurgery), akieleza kuwa ni heshima kubwa kwa Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huo muhimu barani Afrika.
“Serikali imeendelea kuwekeza katika sekta ya afya kwa kuongeza wataalamu wa ubingwa na ubobezi, pamoja na kuboresha miundombinu ya hospitali ili kuhakikisha huduma bora zinawafikia wananchi wengi zaidi”,Amesema Rais Samia.
Ameongeza kuwa kufanyika kwa mkutano huo nchini kunaashiria kukua kwa mchango wa Afrika katika maendeleo ya sekta ya afya duniani, huku akibainisha kuwa Tanzania imeendelea kujijengea heshima katika utoaji wa huduma za kibingwa.
Aidha, Rais Samia amewashukuru wataalamu wa ndani na nje ya nchi kwa kujitoa kuwahudumia wagonjwa wenye uhitaji wa huduma za upasuaji wa ubongo kwani hatua hiyo ni muhimu katika kuokoa maisha ya wananchi.
Ameeleza kuwa upasuaji wa ubongo ni moja ya taaluma nyeti na ya juu inayohitaji utaalamu mkubwa, vifaa vya kisasa pamoja na uwekezaji endelevu ili kukabiliana na changamoto za magonjwa ya mfumo wa fahamu.
Amesema idadi ya madaktari bingwa wa upasuaji wa ubongo imeongezeka kwa kiasi kikubwa kutokana na juhudi za Serikali kupitia programu mbalimbali za mafunzo, ikiwemo ufadhili wa masomo na ushirikiano na taasisi za kimataifa.
Rais Samia amebainisha kuwa pamoja na mafanikio hayo, bado kuna changamoto kubwa zinazohitaji ushirikiano wa wadau mbalimbali, ikiwemo ajali za barabarani ambazo zimeendelea kuwa chanzo kikubwa cha majeraha ya ubongo nchini.
Amesema takwimu zinaonesha kuwa ajali hizo zinachangia kwa kiasi kikubwa vifo na ulemavu, hivyo kuna umuhimu wa kuimarisha usalama barabarani pamoja na kuwekeza zaidi katika huduma za dharura.
Katika hatua nyingine, Rais Samia amesema Serikali inaendelea kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa kuanzisha mifumo ya bima ya afya kwa wote na kuimarisha upatikanaji wa vifaa tiba kupitia Bohari ya Dawa (MSD).
Kwa upande wake, Waziri wa Afya,Mohamed Mchengerwa amempongeza Rais Samia kwa juhudi zake katika kuimarisha sekta ya afya, akisema uwekezaji uliofanywa umeongeza upatikanaji wa huduma na kuleta matumaini kwa Watanzania.
Sambamba na hayo Rais Dk.Samia amekabidhiwa tuzo maalum ya kibinadamu kwa kutambua mchango wake mkubwa katika kuboresha sekta ya afya nchini na Afrika kwa ujumla.
Mkutano huo wa siku tatu unawakutanisha wataalamu na wabobezi kutoka mataifa mbalimbali duniani kwa lengo la kubadilishana uzoefu, maarifa na teknolojia za kisasa katika kuboresha huduma za afya hususan upasuaji wa ubongo.

