Mwamvua Mwinyi, Kibaha
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kibaha, Mwajuma Nyamka, amewaelekeza viongozi wa kata na mitaa katika kata ya Visiga kuhakikisha taka zilizopo katika dampo la muda la Visiga B zinaondolewa haraka ili kuondoa kero kwa wananchi, hasa kipindi hiki cha mvua.
Akizungumza katika ziara yake ya kata kwa kata wilayani humo kwa lengo la kushukuru wananchi kwa kuichagua CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, Nyamka pia aliwataka viongozi wa chama kutoka maofisini na kwenda kusikiliza na kuwahudumia wananchi .
“Tunashukuru Serikali kwa kusimamia utekelezaji wa ilani kwa zaidi ya asilimia 90 na kuendelea kutekeleza miradi ya maendeleo inayogusa maisha ya wananchi,” alieleza Nyamka.
Katika hatua nyingine, Nyamka aliwataka maofisa maendeleo kuendelea kutoa elimu kwa wanawake kuhusu vigezo na utaratibu wa kupata na kurejesha mikopo ili waweze kunufaika na fursa zilizopo.
Vilevile aliwahamasisha wananchi Visiga kujitokeza kwa wingi Aprili 21, 2026 katika Shule ya Msingi Visiga kuupokea Mwenge wa Uhuru utakaowasili katika Manispaa ya Kibaha ukitokea Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha.
Kadhalika aliwataka wananchi kutumia fursa ya uwepo wa wataalamu kutoka Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) anaoambatana nao ili kupata huduma mbalimbali ikiwemo usajili na upatikanaji wa vyeti vya kuzaliwa.
Diwani wa kata ya Visiga, Mohamed Mpaki, alieleza kuwa tangu baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, Serikali imepeleka zaidi ya shilingi milioni 339 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi minne ya maendeleo.
Alitaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na mradi wa maji wa Saeni uliotekelezwa kwa asilimia 75, ujenzi wa madarasa na upatikanaji wa madawati katika Shule ya Sekondari Visiga pamoja na shule za msingi Zegereni.
Hata hivyo, Mpaki alibainisha changamoto zinazoikabili kata hiyo kuwa ni pamoja na tatizo la dampo linalotumika katika eneo binafsi, uwepo wa mzabuni mmoja wa ukusanyaji taka, vitendo vya wizi na udokozi na uharibifu wa barabara unaosababishwa na mvua.
Aliongeza kuwa licha ya Halmashauri kutenga shilingi milioni 30 na baadaye kuongeza hadi milioni 50 kwa ajili ya kata hiyo yenye mitaa saba, fedha hizo bado hazitoshelezi kukidhi mahitaji yaliyopo.
Naye Balozi wa shina namba 6 Visiga B, Rehema Chilambo, alitaja changamoto ya wanawake kukosa mikopo pamoja na kero ya mlundikano wa taka kuwa ni miongoni mwa matatizo yanayohitaji ufumbuzi wa haraka.




