Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, akizungumza wakati wa maadhimisho ya siku ya haki za mlaji Duniani yaliyofanyika kwenye hoteli ya Johari Rutana jijini Dar es Salaam Aprili 02, 2026.

Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya Ushindani (FCC), Agrey Mulimuka, akizungumza katika maadhimisho hayo.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Bi. Khadija Ngasongwa, akielezea mikakati ya FCC katika kutoa elimu ya haki za. mlaji. 

………..

Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, amesema serikali inaendelea kuimarisha mifumo ya ulinzi wa haki za mlaji ili kuhakikisha Watanzania wanapata bidhaa na huduma zenye ubora unaokidhi viwango vilivyowekwa.

Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Haki za Mlaji Duniani yaliyofanyika katika Johari Rotana, Kapinga alieleza kuwa serikali imeweka mkazo katika kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu haki zao wanaponunua bidhaa au kupata huduma.

Alisema kuwa pamoja na mafanikio yaliyopatikana, bado kuna changamoto za baadhi ya wafanyabiashara kutofuata taratibu, hali inayoweza kuwaathiri walaji, hivyo akaonya kuwa hatua kali za kisheria zitaendelea kuchukuliwa dhidi ya watakaokiuka sheria.

Aidha, alibainisha kuwa maendeleo ya teknolojia yameleta fursa na changamoto mpya, hususan katika biashara za mtandaoni, hivyo ni muhimu kwa wadau wote kuhakikisha wanazingatia misingi ya uaminifu na uwazi katika utoaji wa huduma.

Kapinga aliongeza kuwa serikali kupitia taasisi zake itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kutoa elimu kwa umma, ili kuwasaidia walaji kufanya maamuzi sahihi na kuepuka udanganyifu katika masoko.

Pia aliwahimiza watumiaji wa bidhaa na huduma kutoa taarifa pale wanapokutana na changamoto, akisisitiza kuwa ushiriki wao ni muhimu katika kuboresha mifumo ya ulinzi wa haki za mlaji nchini.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya Ushindani (FCC), Agrey Mulimuka, amesema kuwa haki za mlaji ni msingi muhimu katika kulinda ustawi wa wananchi na kuhakikisha soko linafanya kazi kwa ufanisi.

Alisema watumiaji wanapaswa kupewa taarifa sahihi, bidhaa bora na huduma zenye viwango vinavyokubalika, huku akisisitiza kuwa FCC itaendelea kutoa elimu kwa umma ili kuwajengea uwezo wa kutambua haki zao.

Aliongeza kuwa katika dunia ya sasa ya kidijitali, watumiaji wanapaswa kuwa makini zaidi, hasa katika matumizi ya mitandao na huduma za mtandaoni, huku akiwataka watoa huduma kuzingatia sheria na kanuni za ushindani.

Aidha, alisisitiza kuwa ushirikiano kati ya taasisi, wafanyabiashara na watumiaji ni muhimu katika kulinda haki za mlaji, akibainisha kuwa hatua madhubuti zinahitajika zaidi ya malalamiko pekee.

Katika kuongeza msisitizo wake, alisema FCC itaendelea kuimarisha usimamizi wa masoko ili kudhibiti vitendo vya udanganyifu na bidhaa zisizokidhi viwango.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Bi. Khadija Ngasongwa, alisema bado kuna umuhimu mkubwa wa kuendelea kutoa elimu kwa walaji kutokana na wengi kutofahamu haki zao za msingi wanaponunua bidhaa na kutumia huduma.

“Kwa kuwa tukio hili linaendelea hivi sasa, tunaendelea kulitumia kama jukwaa la kuelimisha walaji na wadau mbalimbali kuhusu haki zao, kwa sababu wananchi wengi bado hawana uelewa wa kutosha,” alisema.

Alifafanua kuwa elimu hiyo inalenga kuwajengea wananchi uwezo wa kutambua bidhaa salama na huduma bora, sambamba na kujiepusha na udanganyifu unaoweza kujitokeza sokoni.

Bi. Ngasongwa aliongeza kuwa FCC inaendelea kufanya kampeni za uelimishaji katika mikoa mbalimbali kupitia vipindi vya redio, mihadhara ya umma na majadiliano na wadau.

Aidha, alisisitiza kuwa mlaji mwenye uelewa ana nafasi kubwa ya kujilinda dhidi ya bidhaa duni na huduma zisizo bora.

Alimalizia kwa kuwataka wananchi kutumia fursa ya maadhimisho hayo yanayoendelea kujifunza na kuwa mabalozi wa haki za walaji katika jamii.