Na. Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog, Dodoma
Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Mhe. Godfrey Kasekenya, amesisitiza umuhimu wa Watumishi kufuatilia afya zao ya akili, kuepuka msongo wa mawazo, na kujiandaa kibiashara ili kupata kipato cha ziada na maisha bora baada ya kustaafu.
Akizungumza Machi 31, 2026 jijini Dodoma wakati akifunga wa Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Ujenzi, , Mhe. Kasekenya amesema dhamana ya wajumbe ni kuwakilisha Watumishi wenzake na kurejesha maazimio mbalimbali ili kutekeleza wajibu ipasavyo na kufikia matarajio ya Wizara.
Aidha, amesema mada zinazohusu Udhibiti wa Msongo wa Mawazo, Elimu ya Afya ya Akili, Ujasiriamali na Ajira ni muhimu sana kwa Watumishi wa Umma kutokana na mazingira ya kazi. “Mada hizi zinafundishwa ili ziweze kuwasaidia Watumishi kuwekeza kwa njia ya ujasiriamali na kuwaandaa kwa maisha ya kustaafu,” amesema Mha. Kasekenya
Mhe Mha. Kasekenya amebainisha kuwa mwaka huu Baraza limefanyika kwa vikao viwili, kikiangazia tathmini ya utekelezaji wa bajeti ya Wizara ya mwaka wa fedha 2025/26 na majadiliano ya bajeti ya mwaka wa fedha 2026/27. Amesema majadiliano hayo yamelenga utekelezaji wa majukumu ya Wizara pamoja na maslahi na maendeleo ya watumishi.
Naibu Waziri Mha. Kasekenya amesisitiza watumishi wote kuendelea kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na weledi, huku wakiweka adhma ya Serikali ya awamu ya sita ya kuacha tabasamu kwa wananchi mwishoni mwa utawala wake, na kuwataka kuepuka vitendo vya rushwa na matumizi mabaya ya ofisi.
Awali akizungumza, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Dkt. Charles Msonde, amebainisha kuwa kikao cha Baraza la Wafanyakazi kililenga kusikiliza hoja mbalimbali za matumizi, kujadili kwa kina na kutoa ufumbuzi pamoja na mwelekeo mpya kwa watumishi. Ameeleza kuwa baraza limepata faida kubwa kwa kupitisha mada muhimu ikiwemo uwekezaji na ujasiriamali kwa watumishi, ambapo hata mtumishi mwenye mshahara mdogo anaweza kuimarisha hali yake kifedha na kuwa mwekezaji mzuri.
Aidha, amebainisha kuwa baraza lilijadili lishe bora na afya ya mwili, kujua nini na wakati gani wa kula ili kuimarisha afya na mstakabali wa watumishi, pamoja na afya ya akili, ikiwemo kuepuka msongo wa mawazo ili kuwa na utumishi bora. Pia, wajumbe walijadili mikakati ya ujenzi, kuangalia barabara, madaraja, ukarabati wa miundombinu, na mbinu za kushirikisha sekta binafsi pamoja na kuimarisha vipimo vya mizani ili kuhakikisha ubora wa barabara.
Mkutano wa Baraza la wafanyakazi umetematishwa Leo Ambapo ulianza Machi 30, 2026 .
