NA DENIS MLOWE IRINGA 

MKUU wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, amesema maandalizi ya mazishi ya aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Isimani na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), William Lukuvi, yanaendelea vizuri, huku Serikali ikihakikisha kuwa taratibu zote za kitaifa zinafuatwa.

Akizungumza kijijini Idodi, ambako marehemu anatarajiwa kuzikwa Machi 31, 2026, RC James alisema Serikali kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama imejipanga kuhakikisha shughuli zote za kuaga na mazishi zinakwenda kwa utulivu na heshima inayostahili.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa, maandalizi ya miundombinu katika maeneo yote muhimu ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Iringa na kijiji cha Idodi yanaendelea vizuri, ikiwa ni pamoja na maandalizi ya kupokea maelfu ya waombolezaji kutoka maeneo mbalimbali.

Alisema siku ambayo mwili wa marehemu utafikishwa Idodi, kutakuwa na maeneo matatu makuu ya kusimama ili wananchi wa njia na vituo mbalimbali wapate fursa ya kumuaga kiongozi huyo aliyelitumikia Taifa kwa muda mrefu. 

Aidha, baada ya mwili kuwasili nyumbani, kutafanyika maombolezo ya pamoja usiku huo kabla ya misa na mazishi kufanyika siku inayofuata asubuhi.

Mkuu wa Mkoa aliwashukuru viongozi wa vijiji, vitongoji, kata na tarafa ya Idodi kwa ushirikiano mkubwa wanaoutoa kwa familia na Serikali katika maandalizi hayo, na akatoa wito kwa wananchi kushiriki kwa mujibu wa ratiba.

“Maandalizi yanaendelea vizuri, na tuna imani ratiba iliyotangazwa itatekelezwa kama ilivyopangwa. Serikali imejipanga kuhakikisha kila hatua inaenda sambamba na taratibu za kitaifa,” alisema RC James.

Mazishi ya Lukuvi, ambaye pia aliwahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Ismani, yanatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi wa kitaifa, ndugu, jamaa na wananchi kutoka maeneo mbalimbali nchini.