Na Mwandishi Wetu
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imetoa msaada wa mashine mbili za kisasa kwa ajili ya kutoa joto kwa watoto njiti katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Amana, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha huduma za afya nchini.
Msaada huo unalenga kuokoa maisha ya watoto wanaozaliwa kabla ya wakati kwa kuwapatia huduma muhimu ya joto, ambayo ni ya msingi katika hatua za awali za uhai wao.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Crispin Chalamila, amesema hatua hiyo ni mwendelezo wa taasisi hiyo kurejesha kwa jamii kupitia michango ya watumishi wake.
“Mpaka sasa tayari tumefikia hospitali 17 kati ya 26, na tunaendelea kuhakikisha tunagusa maeneo yenye uhitaji mkubwa zaidi,” amesema Chalamila.
Ameongeza kuwa TAKUKURU imeona umuhimu wa kuwagusa watoto njiti ambao wanahitaji uangalizi wa karibu ili kuongeza nafasi ya kuishi.
Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Amana, Jumanne Ihoyelo, amesema mashine hizo zitasaidia kupunguza changamoto ya upatikanaji wa vifaa tiba na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa watoto njiti.
“Vifaa hivi vitasaidia kuboresha huduma na kupunguza vifo vya watoto njiti vinavyoweza kuzuilika,” amesema Ihoyelo.
Naye Muuguzi Mwandamizi wa wodi ya watoto, Mary Machemba, ameishukuru TAKUKURU kwa msaada huo, akieleza kuwa utasaidia kuokoa maisha ya watoto wengi zaidi.
Ametoa wito kwa wadau wengine kujitokeza kusaidia sekta ya afya ili kuimarisha huduma kwa watoto na makundi mengine yenye uhitaji mkubwa.

TAKUKURU YATOA MASHINE ZA KUHUDUMIA WATOTO NJITI HOSPITALI YA AMANA
