Na John Walter -Babati
Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini na Naibu Spika, Daniel Sillo, ameendelea kuonesha dhamira yake ya kuboresha sekta ya elimu kwa kukabidhi mashine ya kudurufu mitihani katika Shule ya Sekondari Ayatsea.
Makabidhiano ya mashine hiyo yamefanyika kupitia Katibu wa CCM Babati Vijijini, Aziza Isimbulla, ambaye alimwakilisha mbunge huyo katika hafla hiyo.
Akizungumza wakati wa tukio hilo, Isimbulla amesema chama hicho kinafurahishwa na utekelezaji mzuri wa ilani ya CCM unaofanywa na Sillo, hasa katika sekta ya elimu.
Amesema kuwa hatua ya mbunge huyo kutumia sehemu ya mshahara wake binafsi kununua mashine za kudurufu mitihani na kuzigawa katika shule mbalimbali ni mfano wa uongozi wa kujitolea na unaolenga kuleta matokeo chanya kwa jamii.
“Tunaona kwa vitendo utekelezaji wa ilani ya chama chetu, na hii ni ishara ya kujali maendeleo ya wanafunzi na walimu,” amesema Isimbulla.
Hafla hiyo ya makabidhiano pia ilishuhudiwa na Katibu wa Mbunge huyo, Waziri Juma, pamoja na viongozi wengine wa chama na elimu katika eneo hilo.
Hatua hiyo inatarajiwa kusaidia kurahisisha uandaaji na uchapishaji wa mitihani shuleni hapo, na hivyo kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji kwa wanafunzi.
