………..
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Kuendelelea kutupwa kwa nyavu zilizoisha na taka za nguo ndani ya Ziwa Victoria kumeelezwa kuwa ni mojawapo ya chanzo kinachosababisha athari kwa mazalia ya samaki.
Akizungumza jana na Vyombo vya Habari Jijini Mwanza Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Blue Victoria, Festus Masahho alisema taka hizo huzuia samaki kuzaliana ndani ya ziwa hivyo kusababisha upungufu unaoshuhudiwa kuwepo kwa sasa.
Alisema taka hizo hufunika katika mchanga ambapo ndo samaki huingia kwa ajili ya kutaga mayai wakati huo huo ukisababisha kunaswa na hivyo kushindwa kuondoka maeneo hayo na kufa.
Masahho aliendelea kusema kuwa taka hizo zinazoingia ndani ya ziwa husababisha uchafuzi wa maji na kukinga mwanga ambao ni mhimu kwa maisha ya samaki na kuharibu mayai ya samaki yanayotagwa kwa kuzuia kuanguliwa.
Aidha aliongeza kwa kusema kuwa madhara mengine yanayojitokeza kutokana na taka hizo ziingiazo ziwani ni kuzuia kwa kukinga uwepo wa hewa ya okisijeni ambayo ni mhimu kwa maisha ya samaki.
Aidha Masahho alisema wameanza kutembelea maeneo ya uvuvi katika mialo ya Bezi, Kayenze na Igombe zilizopo katika Manispaa ya Ilemela kutoa elimu kuteketeza nyavu na taka zilizotupwa kwa kuzitoa ziwani.
Alisema wataendelea kupita katika mialo mingine iliyobakia katika Manispaa ya Ilemela ili kuzungumza na Kamati za Usimamizi wa Mialo (BMU) na wavuvi ili waweze kuchukua tahadhari dhidi ya utupaji wa taka hizo zenye madhara kwa maisha ya samaki.
“Wavuvi wananunua nyavu kila siku lakini hawana taarifa zinazoonesha zilizoisha wameziteketeza hivyo tunataka wawe na takwimu wameteketeza wapi” alisema Masahho.
Alitoa wito kwa wavuvi kuchukua tahadhari ili kuondoa changamoto ya kuisha kwa samaki kwani taka zinaendelea kusababisha sehemu za kutagia mayai kupungua, samaki wadogo kuhangaika katika ukuaji wake.
Aidha alihitimisha kwa kuomba jamii kuepuka utupaji hovyo wa taka kwa kujenga utamaduni wa kuwa na sehemu maalumu ya kutupia ili uchafu huo usiingie ziwani na kuharibu mfumo wa ekolojia ya viumbe hao.