
Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo (kulia) akiwa na Makamu wa Rais wa Chuo Kikuu cha Limerick Profesa Colin Fitzpatrick (kushoto) wakisaini hati ya makubaliano yenye lengo la kuendeleza ushirikiano katika utoaji wa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wa kitanzania, waliosimama ni Balozi wa Ireland nchini Tanzania, Mhe. Nicola Brennan, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda katika hafla fupi iliyofanyika leo Machi 26, 2026 katika Ukumbi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda akizungumza katika hafla ya utiaji saini hati ya wakisaini hati ya makubaliano yenye lengo la kuendeleza ushirikiano katika utoaji wa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wa kitanzania.

…………..
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeingia makubaliano na Chuo Kikuu cha Limerick cha Ireland ili kuwapatia vijana wa Kitanzania fursa ya kusoma katika chuo hicho kwa punguzo la ada la asilimia 50 ambao ni mpango wa kimkakati unalenga kuwajengea vijana ujuzi katika teknolojia zinazoibukia.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Machi 26, 2026, jijini Dar es Salaam baada ya hafla ya utiaji saini wa makubaliano hayo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema kuwa hatua hiyo itatoa nafasi za masomo kwa wanafunzi waliofanya vizuri katika masomo ya sayansi kupitia Samia Scholarship.
Profesa Mkenda amesema kuwa makubaliano hayo yatasaidia kuimarisha ushirikiano wa kitaasisi kati ya Wizara na Chuo Kikuu cha Limerick, pamoja na kukuza ubadilishanaji wa maarifa, tafiti za pamoja na ujenzi wa uwezo.
Ameongeza kuwa mwaka 2025, wanafunzi 50 walishiriki mafunzo ya awali (bootcamp) katika NM-AIST, huku wanafunzi 32 wakiendelea na masomo katika Chuo Kikuu cha Limerick katika fani mbalimbali zikiwemo Akili Unde (Artificial Intelligence), Sayansi ya Kompyuta, Uhandisi wa Elektroniki na Sayansi za Hisabati.
“Natoa shukrani za dhati kwa uongozi wa Chuo Kikuu cha Limerick kwa kujitolea kupokea wanafunzi wa Kitanzania. Pia, ushirikiano kati ya COSTECH na wadau wengine umeonesha uhusiano imara unaoendelea kukua,” amesema Profesa Mkenda.
Amebainisha kuwa Serikali ya Tanzania, kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na taasisi zake, inaendelea kutekeleza Programu ya Samia Scholarship Extended inayojikita katika Sayansi ya Data, Akili Unde na taaluma zinazohusiana.
Kwa upande wake, Makamu wa Rais Chuo Kikuu Cha Limerick Profesa Colin Fitzpatrick, amesema kuwa wataendelea kushirikiana na Tanzania katika sekta mbalimbali, hususan elimu, ili kuhakikisha malengo yaliyokusudiwa yanafikiwa.
Ushirikiano huo unaendana na vipaumbele vya taifa vya kuendeleza sayansi, teknolojia na ubunifu, pamoja na kujenga rasilimali watu yenye ujuzi wa hali ya juu na kuiweka Tanzania katika nafasi nzuri ndani ya uchumi wa kidijitali wa dunia.
