Na Mwandishi Wetu, Mbinga
Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Kisare Makori, amekabidhi mifuko 750 ya mbolea aina ya DAP yenye thamani ya shilingi 63,000,000 kwa walimu wakuu wa shule za msingi na sekondari wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga zilizotolewa kwa lengo la kuimarisha utunzaji wa miche ya kahawa iliyopandwa katika mashamba ya shule.
Mkakati huo wa kupanda Kahawa umeanzishwa na Mkurugenzi ili kuziwezesha shule kujitegemea kiuchumi.
Mbolea hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga (DED), ikiwa ni mwendelezo wa mkakati wa wilaya hiyo kurejesha hadhi ya zao la kahawa na kufundisha wanafunzi elimu ya kujitegemea kupitia shughuli za kilimo katika mazingira ya shule.
DC Makori alisema kuwa,Halmashauri ya wilaya Mbinga inachagiza maono ya Serikali ya wamu ya sita kukuza uchumi kwa kuwekeza nguvu kwenye zao la kahawa.
“Nimesikia kahawa imechangia zaidi ya asilimia 50 ya mapato yote ya makusanyo kwa msimu uliopita kwa hiyo tunapopanua wigo wa zao la kahawa tunaongeza kipato.”alisema DC Makori.
DC Makori aliongeza kuwa, shule zinapokuwa na uwezo wa kujitegemea kwa kipato zinaweza kufanya mapinduzi katika kuboresha miundombinu ya shule kupitia mapato ya ndani.
” Tunao mfano mzuri shule yetu ya Sekondari Kigonsera ambayo imetumia mapato yake ya ndani kujenga nyumba za walimu,zipo shule nyingi zinazotumia mapato ya ndani kufanya miradi ya maendeleo,ni matumaini yangu kuwa mradi huu wa kahawa utawezesha shule nyingi kujitegemea kiuchumi”alisisitiza Makori.
Akito taarifa ya mpango wa kuongeza uzalishaji wa mapato yatokanayo na zao la kahawa Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga Andrew Mbunda alisema, katika msimu wa 2025/2026 zao la kahawa limeiwezesha Halmashauri kukusanya jumla ya Shilingi 6,630,187,816 kutokana na uzalishaji wa tani 18,925 ambapo wastani wa bei ulikuwa shilingi 11,200 kwa kilo.
Naye Mkuu wa shule ya Sekondari Kigonsera Ponsiano Ngungulu alisema kuwa,mpango wa kupanda kahawa kila shule ni maono mazuri ili shule zijitegemee kiuchumi na amemshukuru Mkurugenzi kwa kuwapatia mbolea.