
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Bw. Hamad Abdallah (kushoto) akito taarifa ya utekelezaji wa mradi Housing Scheme Kawe wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) ilipofanya ziara ya ukaguzi wa mradi huo Leo Machi 25, 2025 Jijini Dar es Salaam.


Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) Mhe. Massanja Kagodogosa akizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Bw. Hamad Abdallah wakati wakikagua mradi wa Housing Scheme Kawe.

Msimamizi wa utekelezaji wa mradi wa Samia Housing Scheme Kawe, Mhandisi Grace Musita (kushoto) akitoa taarifa utekelezaji wa mradi huo Kwa PIC
…….
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) imefanya ziara ya ukaguzi wa mradi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Samia Housing Scheme uliopo Kawe, Dar es Salaam.
Hata hivyo, walishindwa kuendelea na ukaguzi wa mradi mwingine wa Kawe 711 baada ya kupokea taarifa ya kifo cha aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) na Mbunge wa Jimbo la Isimani, William Lukuvi (70), ambaye amefariki dunia leo asubuhi katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, jijini Dodoma, alipokuwa akipatiwa matibabu.
Akizungumza leo Machi 25, 2026 wakati akitoa taarifa ya mradi wa Samia Housing Scheme Kawe, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Bw. Hamad Abdallah, amesema kuwa mradi huo una maghorofa kumi yenye jumla ya nyumba 560, na unatekelezwa na wahandisi wa ndani kutoka NHC.
Akitoa ufafanuzi wa mradi huo, Msimamizi wa utekelezaji wa mradi wa Samia Housing Scheme Kawe, Mhandisi Grace Musita, amesema kuwa maghorofa hayo yana nyumba za vyumba vitatu zenye ukubwa wa mita za mraba 89, ambazo zimeuzwa kwa shilingi milioni 192.7.
Amesema pia kuna nyumba 160 za vyumba viwili zenye ukubwa wa mita za mraba 68, ambazo zimeuzwa kwa shilingi milioni 147, huku nyumba ndogo zenye mita za mraba 21.2 zikiuzwa kwa shilingi milioni 38.8.
Mhandisi Musita amesema kuwa mradi huo ulioanza Novemba 2022 ulikamilika Juni 2025, na kwa sasa wateja tayari wameanza kuishi, huku shirika likiwa katika hatua za kukamilisha dosari ndogondogo zinazojitokeza.
Amefafanua kuwa mradi wa Samia Housing Scheme Kawe umekuwa wa kipekee kwani umeweza kutengeneza ajira 11,800 kwa mafundi mbalimbali, wakiwemo wanafunzi wa vyuo vya ufundi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT).
Aidha, amesema wanafunzi 630 walipata mafunzo katika mradi huo, wakiwemo 47 waliopata ajira za kudumu na za muda mfupi. Pia, vibarua 100 wasio na elimu rasmi lakini wenye nidhamu na ufanisi walipata ajira katika mradi huo.
Hata hivyo, Kamati hiyo ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Massanja Kagodogosa, ilishindwa kuendelea kukagua mradi wa Kawe 711 baada ya kupokea taarifa ya kifo cha William Lukuvi.
