Kamati ya utekelezaji wa mradi wa Kukuza Usawa wa Kijinsia Tanzania (PAMOJA) inayoundwa na wajumbe kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum pamoja na viongozi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imekutana kwa lengo la kupitia taarifa ya utelekezaji wa mradi kwa kipindi cha robo ya pili pamoja na maandalizi ya mpango wa makadirio ya bajeti ya mradi ya mwaka 2026/2027.
Kikao kazi hicho kimefanyika leo tarehe Machi 25, 2026 jijini Dodoma, kikiongozwa na Mkurugenzi wa Mipango wa Wizara ya Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Victor Nkiya, ambapo wajumbe wamepata fursa ya kupitia taarifa za utekelezaji na kujadili mapendekezo ya bajeti ya mwaka 2026/2027.
Utekelezaji wa mradi huu umejikita katika maeneo manne ambayo ni kuongeza upatikanaji wa fursa za kiuchumi kwa wanawake, Huduma za kuzuia na kutokomeza ukatili wa kijinsia, kuimarisha ubunifu na ushirikiano pamoja na usimamizi wa mradi, ufuatiliaji na Tathimini.

