Na. Fullshangwe Blog.
Mratibu wa Kifua Kikuu na Ukoma Wilaya ya Siha, Michael Mushi, ameitaka jamii kuchukua hatua za haraka pindi wanapobaini mtu mwenye dalili za kifua kikuu kwa kumpeleka katika kituo cha afya kilicho karibu kwa uchunguzi na matibabu.
Amesema huduma za uchunguzi na matibabu ya kifua kikuu zinatolewa bure, hivyo hakuna sababu ya kuchelewa kutafuta tiba.
“Tunaiasa jamii, mtu yeyote akionekana na dalili za kifua kikuu apelekwe mapema hospitali kwa uchunguzi,huduma hizi ni bure kabisa,” amesema Mushi.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuondoa dhana potofu zilizojengeka miongoni mwa wananchi kuwa kifua kikuu ni ugonjwa wa kurithi au wa kurogwa.
“Kifua kikuu si ugonjwa wa kurithi wala kurogwa ni ugonjwa unaoambukizwa kwa njia ya hewa, hivyo mtu yeyote anaweza kuambukizwa,” alieleza.
Katika hatua nyingine, Mushi ametoa wito kwa jamii kuacha unyanyapaa dhidi ya wagonjwa wa kifua kikuu, akibainisha kuwa mgonjwa anapoanza matibabu hupunguza uwezekano wa kuwaambukiza wengine na hatimaye hupona kabisa
“Mgonjwa akianza matibabu hana uwezo tena wa kusambaza ugonjwa. Akimaliza dozi anapona na anarudi kuishi maisha ya kawaida kama wengine,” alisisitiza.
Kwa upande wa takwimu, Wilaya ya Siha imeendelea kuimarisha mapambano dhidi ya TB ambapo katika mwaka uliopita jumla ya wagonjwa 752 waligundulika na kuanza matibabu.
Hata hivyo, kati ya wagonjwa hao, watoto 127 wenye umri chini ya miaka 14 walibainika kuwa na maambukizi, hali inayozua tahadhari zaidi kwa jamii kulinda kundi hili.
Akizungumzia hali hiyo, wataalamu wa afya wameeleza kuwa watoto huambukizwa zaidi kutoka kwa watu wazima wanaoishi nao karibu kama wazazi, walezi au katika mazingira ya shule.
“Watoto wengi huambukizwa kutoka kwa watu wazima walioko karibu nao, hivyo uchunguzi wa mapema na tahadhari ni muhimu sana,” aliongeza.
Wilaya hiyo ina vituo mbalimbali vya afya vinavyotoa huduma za TB, vikiwemo vya serikali, taasisi za dini na binafsi, ambapo wananchi wote wanapata huduma hizi bila malipo.
