Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), Prof. Joseph C. Ndunguru, akizungumza na waandishi wa habari Machi 24,2026 kuhusu miradi ya maendeleo na fursa kwa vijana, katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.
Na. Meleka Kulwa- Fullshangwe Blog, Dodoma
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), Prof. Joseph C. Ndunguru, amesema kuwa mamlaka hiyo imenunua ndege nyuki za kisasa kwa ajili ya kuboresha ufuatiliaji na udhibiti wa visumbufu vya mazao mashambani.
Amesema kuwa kwa sasa wana jumla ya ndege nyuki 21 na wako katika hatua za kukamilisha ununuzi wa ndege nyuki nyingine 20.
amesema hayo Machi 24, 2026, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu miradi ya maendeleo na fursa kwa vijana, katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.
Amesema kuwa hatua hiyo itafanya idadi ya ndege nyuki kufikia 41.
Aidha amebainisha kuwa ndege hizo aina ya Havilland zitatumika kupita katika mashamba ya wakulima kwa ajili ya kuchunguza viashiria vya visumbufu.
Aidha amebainisha kuwa lengo ni kudhibiti visumbufu hivyo kabla havijasababisha madhara kwa wakulima.
Pia ameongeza kuwa baadhi ya ndege hizo zina uwezo wa kunyunyizia viuatilifu katika eneo la hekta 52 kwa saa.
Ameongeza kuwa mamlaka imenunua pia ndege ya kisasa ya kunyunyizia viuatilifu aina ya Thrush 510 yenye uwezo wa kubeba lita 1,930 za viuatilifu na tenki la mafuta la lita 863.
Aidha amesema kuwa ndege hiyo ina uwezo wa kunyunyizia viuatilifu katika eneo la ekari 2,400 kwa wakati mmoja na ni ya kipekee katika ukanda wa Afrika Mashariki, huku akibainisha kuwa taratibu zote za usajili wake zimeshakamilika ikiwemo kupata ithibati kutoka serikalini.


