Taasisi ya Jumuiya ya Tabia za Kiislamu (JAI) imewafariji wagonjwa zaidi ya 1,800 katika hospitali mbalimbali, ikiwemo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, wakati wa sikukuu ya Eid al-Fitr. Hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za kuwapa faraja na kuwafanya wajione kuwa sehemu ya jamii licha ya changamoto za kiafya wanazopitia.

Akizungumza leo, Machi 21, 2026, jijini Dar es Salaam katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili wakati wa zoezi la kugawa chakula kwa wagonjwa, Katibu wa JAI, Ramadhani Kombo, amesema lengo la taasisi hiyo ni kuhakikisha wagonjwa wanasherehekea sikukuu hiyo kwa furaha kama Watanzania wengine.

Amesema kuwa wamefanikiwa kuwafikia wagonjwa zaidi ya 1,800 kwa kuwapatia chakula maalum cha sikukuu.

“Lengo letu ni kusherehekea sikukuu pamoja na wagonjwa ili nao wajione kuwa ni sehemu ya Watanzania, kwani maradhi ni mitihani ya maisha,” amesema Kombo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa JAI, Ridhiwani Mpanju, amesema kuwa taasisi hiyo ilianzishwa mwaka 2008 kabla ya kusajiliwa rasmi mwaka 2014, ikiwa na dhamira ya kuwahudumia wagonjwa na kuwapa faraja katika kipindi wanachopitia changamoto za kiafya.

Amesema kuwa kupitia makao makuu ya jumuiya hiyo yaliyopo Magomeni, wamekuwa wakitekeleza shughuli mbalimbali za kijamii, ikiwemo kuwapatia wagonjwa uji wa asubuhi na chakula cha kufuturu wakati wa mwezi wa Ramadhani, pamoja na kusaidia kulipia bili za wagonjwa waliokwama hospitalini.

Viongozi wa jumuiya hiyo wamewaomba waumini wa dini ya Kiislamu pamoja na wadau wengine wa maendeleo kuendelea kuchangia ili kufanikisha lengo la kuwasaidia wagonjwa.