Happy Lazaro,Arusha 

Arusha .Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imeridhishwa na maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Soko la Kilombero katika Jiji la Arusha, ikieleza kuwa kukamilika kwake kutaleta mapinduzi makubwa katika sekta ya biashara na ustawi wa wafanyabiashara wa eneo hilo.

Wajumbe wa kamati hiyo walitembelea na kukagua mradi huo leo ambapo walibaini kuwa ujenzi unaendelea kwa kasi na umezingatia viwango vinavyotarajiwa, hali inayotoa matumaini ya kuboresha mazingira ya biashara ukilinganisha na hali ilivyokuwa awali.

Akizungumza mara baada ya ukaguzi huo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Florent Kyombo (Mb), amepongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya masoko ya kisasa nchini. Alieleza kuwa soko hilo litachochea ukuaji wa uchumi wa Jiji la Arusha kwa kuwapatia wafanyabiashara sehemu salama, yenye hadhi na rafiki kwa shughuli zao.

Amesema masoko ya kisasa kama la Kilombero si tu yanapandisha hadhi ya miji, bali pia yanahakikisha usalama wa wafanyabiashara na wateja, sambamba na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma.

Aidha, Mhe. Kyombo amewataka wananchi wa mkoa wa Arusha kuendelea kumuunga mkono Rais na juhudi za Serikali katika kuboresha maisha ya wananchi, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya wananchi na viongozi wao.

“Niwaombe wananchi, hususan wafanyabiashara, kuendelea kushirikiana na viongozi wa ngazi zote. Lengo ni kuhakikisha mnapata huduma bora na kunufaika na fursa zilizopo,” amesema.Kwa upande wake, Mjumbe wa Kamati hiyo, Mhe. Charles Mahera (Mb), amebainisha kuwa miundombinu ya soko hilo imezingatia viwango vya kisasa na kimataifa, ikijumuisha huduma muhimu za kijamii kama vyumba maalum vya kupumzikia na kunyonyeshea watoto kwa kina mama.

Ameeleza kuwa uwepo wa huduma hizo utasaidia kuboresha afya na ustawi wa watoto, hasa wale wa chini ya miaka mitano, kwa kuwa karibu na mama zao wakati wa shughuli za biashara, hatua itakayochangia pia kupunguza changamoto za lishe duni.

Katika hatua nyingine, wajumbe wa kamati hiyo waliupongeza uongozi wa Mkoa wa Arusha kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo, wakisema utekelezaji wa mradi huo unaonesha ushirikiano thabiti kati ya viongozi wa ngazi mbalimbali za Serikali.

Amefafanua kuwa fedha hizo zinatoka Serikali Kuu kwa ufadhili wa Benki ya Dunia, kupitia mpango wa kuboresha miji na majiji nchini (TACTIC), unaolenga kuinua hadhi ya maeneo ya mijini kwa kuzingatia mahitaji ya kisasa.