Na Silivia Amandius
Bukoba – Kagera
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mheshimiwa Bashiru Ally, amesema wizara yake itaendelea kusimama bega kwa bega na vyama vyote vya ushirika vinavyojihusisha na sekta za kilimo, mifugo na uvuvi ili kuhakikisha vinakua kiuchumi na kuwainua wanachama wake.
Akizungumza Machi 2, 2026 katika ziara ya kukagua miradi iliyotekelezwa kwa ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB), Waziri huyo alisema kuwa hapo awali sekta za mifugo na uvuvi zilikuwa hazipewi kipaumbele na taasisi nyingi za kifedha, hali iliyokuwa inakwamisha ukuaji wake. Amesema serikali ya sasa imeweka mikakati madhubuti ya kuzifanya sekta hizo kuwa kichocheo cha uchumi wa wananchi.
Ameipongeza TADB pamoja na Heifer International kwa kuendelea kuweka mikakati ya kuikuza Maruku AMCOS na kuwasaidia wanachama wake kujikwamua kiuchumi. Pia ameipongeza serikali kwa kuondoa kodi kwenye baadhi ya vifaa vya kuvunia maziwa na mbegu, hatua inayolenga kupunguza gharama za uzalishaji.
Aidha, amezishauri halmashauri zinazotoa mikopo ya asilimia kumi kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kuiga mfumo unaotumiwa na TADB katika utoaji wa mikopo nafuu, ili kuwawezesha wananchi wengi zaidi kuwekeza katika ufugaji, ikiwemo ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba.
Ameitaka Maruku AMCOS kuendelea kuwa mfano bora kwa vyama vingine vya ushirika, akibainisha kuwa chama hicho kwa sasa kinazalisha lita 600 za maziwa kwa siku na kimejiwekea lengo la kufikia lita 1,200 kwa siku katika kipindi kijacho.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TADB, Ndg. Frank Nyabundege, amesema benki hiyo imetoa mkopo wa shilingi milioni 95 kwa wafugaji wa Maruku AMCOS kwa riba nafuu, huku ikitoa pia shilingi milioni 18 kama ruzuku ya kupunguza mzigo wa marejesho. Amewataka wanufaika hao kutumia fedha hizo kwa nidhamu ili kujiimarisha kiuchumi, akisisitiza kuwa soko la maziwa lipo na lina uhakika.
Naye Mark Tsoxo, Mkurugenzi Mkazi wa Heifer International, amesema kwa kushirikiana na TADB wamekuwa wadau wakubwa katika kuwawezesha wakulima na wafugaji kufikiwa kwa urahisi zaidi. Ameeleza kuwa jumla ya mitaji yenye thamani ya shilingi 282,000,000 imesambazwa katika kanda mbalimbali, na watu 42,700 wamefikiwa na programu hiyo. Mkoa wa Kagera pekee, zaidi ya watu 9,000 wamenufaika, huku ng’ombe 300 wakitolewa kupitia mfumo wa “kopa ng’ombe, lipa maziwa,” unaolenga kuongeza mzunguko wa manufaa kwa wanufaika wengine.




