Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Keep a Child Alive, Antonio Ruiz-Giménez Jr. na Ujumbe wake pamoja na Mkurugenzi wa Taasisi ya Doris Mollel Foundation Bi. Doris Mollel, tarehe 1 Machi, 2026 Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Pamoja na masuala mengine mazungumzo hayo yalijikita kuimarisha ushirikiano baina ya Serikali na Taasisi hiyo katika kuboresha huduma za uzazi na afya ya mama na mtoto nchini.

……………
Na Mwandishi Wetu
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo amekutana na ujumbe wa taasisi ya Keep a Child Alive (KCA) ukiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wake, Bw. Antonio Ruiz-Giménez, Jr., katika Ikulu ya Dar es Salaam.
Mazungumzo hayo yalilenga kuimarisha ushirikiano katika kuboresha huduma za uzazi na afya ya mama na mtoto nchini, ambapo pande hizo zimeweka msingi wa ujenzi wa wodi 27 za kisasa za kulelea watoto njiti Tanzania Bara na Zanzibar. Wodi hizo zinatarajiwa kujengwa kwa kuzingatia viwango vya kimataifa ili kukidhi mahitaji ya huduma maalum kwa watoto wanaozaliwa kabla ya wakati.
Mpango huo utatekelezwa kwa ushirikiano na Doris Mollel Foundation, ukiwa na lengo la kuimarisha miundombinu ya afya ya uzazi, kuongeza upatikanaji wa vifaa tiba, na kuchangia kupunguza vifo vya akina mama pamoja na watoto wachanga, hususan watoto njiti.
Akizungumza katika kikao hicho, Rais Dkt. Samia amesema Tanzania imepiga hatua kubwa katika kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi, kutoka vifo 556 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2016 hadi 104 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2022. Aidha, vifo vya watoto chini ya miaka mitano vimepungua kwa asilimia 36, kutoka 67 hadi 43 kwa kila vizazi hai 1,000 katika kipindi hicho.
Ameeleza kuwa mafanikio hayo yametokana na uwekezaji mkubwa wa Serikali katika ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za afya karibu na wananchi, kuajiri watumishi wa afya, pamoja na kuimarisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba vya kisasa.
Hata hivyo, Rais amebainisha kuwa bado ipo changamoto ya kupunguza vifo vya watoto wachanga kutokana na upungufu wa wodi maalum za watoto wachanga. Amefafanua kuwa Serikali imeandaa mpango mkakati wa kujenga wodi 15 za ziada, sambamba na kuimarisha uwezo wa wahudumu wa afya na upatikanaji wa vifaa tiba, ili kuhakikisha watoto wote wanaozaliwa nchini wanapata huduma stahiki na salama.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kimataifa ya Keep a Child Alive, Antonio Ruiz-Giménez Jr. na Ujumbe wake, Naibu Waziri wa Afya Dkt. Florence Samizi pamoja na Mkurugenzi wa Taasisi ya Doris Mollel Foundation Bi. Doris Mollel, tarehe 1 Machi, 2026 Ikulu Jijini Dar es Salaam.
