Mwenyekiti wa Chama cha msingi cha Ushirika Liyombo kilichopo kijiji cha Liyombo Halmashauri ya Wilaya Mbinga Mkoani Ruvuma Joseph Mbele aliyevaa koti jeupe,akimuongoza Afisa Ushirika kutoka Halmashauri ya Wilaya Mbinga Leo Kumburu wa pili kushoto na wanachama wa chama hicho kukagua nyumba ya walimu wa shule ya msingi Liyombo iliyojengwa na Chama hicho ili kusaidia makazi ya walimu.
Na Mwandishi Wetu,Mbinga
CHAMA cha Msingi cha Ushirika Liyombo Amcos kilichopo kijiji cha Liyombo kata ya Linda Halmashauri ya Wilaya Mbinga Mkoani Ruvuma,kimekamilisha ujenzi nyumba moja ya kuishi familia tatu za walimu ili kupunguza uhaba wa nyumba za walimu wa shule ya msingi Liyombo.
Akizungumza jana Mwenyekiti wa chama hicho Joseph Mbele alisema,Chama kimeamua kujenga nyumba hiyo ili kuboresha mazingira ya kufundishia,kujifunzia,kupunguza uhaba wa makazi,kuinua ari ya walimu na kuongeza ufaulu kwa wanafunzi wa shule hiyo.
Alisema,ujenzi wa nyumba hiyo ulianza mwaka 2025 na waliamua kuwekeza nguvu kubwa katika sekta ya elimu kutokana na changamoto kubwa ya makazi bora ya walimu na sehemu ya kurudisha faida kwa jamii kutoka fedha za ushuru kwenye zao la kahawa.
Alisema,baadhi ya walimu wa shule ya msingi Liyombo wanaolazimika kupanga mitaani na kutumia muda mrefu kuwahi kwenye majukumu yao na wengine wanaoletwa kufanya kazi waliamua kukimbia kutokana na miundombinu ya shule kuwa mibaya.
Alisema,mkakati wa Chama hicho kuendelea kuboresha makazi ya walimu kwani baada ya kumaliza nyumba hiyo ambayo zitaishi familia tatu za walimu, wameanza kujenga nyumba nyingine ya Mwalimu Mkuu.
“Pia tunaendelea na ujenzi wa zahanati kijiji ambayo kwa sasa ipo hatu ya kupaua ili iweze kutoa huduma kwa wananchi ambao kwa sasa wanalazimika kwenda vijiji vingine kama Linda makao makuu ya kata na Mkumbi kwa ajili ya kufuata huduma za afya”alisema Mbele.
Akizungumza kwa niaba ya walimu wa shule hiyo Feli John,ameishukuru Liyombo Amcos kujenga nyumba ya kisasa ambayo imepunguza changamoto kubwa ya makazi bora kwa walimu wa shule hiyo.
Mwalimu John,amekiomba Chama hicho kuendelea kuwashika mkono walimu na wanafunzi wa shule hiyo kuboresha mazingira ya shule kwa kujenga nyumba na mdarasa ya kisasa kwani yaliyopo yameanza kuchakaa.
“Kwa niaba ya walimu wote wa shule hii nawashuru viongozi wa Liyombo Amcos kwa kutujengea nyumba hizi ambazo zitawezesha kuishi sehemu salama na bora,ukosefu wa nyumba za walimu shuleni imesababisha athari kubwa ikiwemo walimu kutofika kwa wakati darasani”alisema Mwalimu Feli John.
Mwenyekiti wa Serikali ya kijiji cha Liyombo Nobert Mwingira,ameiomba Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya Mbinga kuunga mkono juhudi zilizoanzishwa na Chama cha msingi cha Ushirika Liyombo kwa kuongeza majengo mapya hasa madarasa ya shule ya msingi ambayo kwa sasa yameanza kuchakaa kwani tangu ilipoanzishwa haijawahi kupata mradi mpya.
Afisa kilimo na ushirika kutoka Halmshauri ya Wilaya Mbinga Leo Kumburu alisema,ujenzi wa nyumba hizo ni mkakati wa Halmashauri ya Wilaya kuhakikisha kila Chama cha Msingi kupitia zao la kahawa kinatenga Sh.20 kwa ajili ya kuendeleza miradi ya maendeleo vijijini.
Alisema,ndiyo maana Liyombo Amcos imetekeleza kwa vitendo mkakati huo kwa kujenga nyumba mbili kwa ajili ya makazi ya walimu wa shule ya msingi Liyombo na ujenzi wa zahanati ya kijiji.
Kumburu,amevitaka vyama vingine vya msingi katika Halmashauri hiyo kuiga mfano wa Liyombo Amcos kwa kurudisha faida kwa jamii na kutumia faida wanayopata kupitia ushuru wa kahawa na mazao mengine kuanzisha miradi itakayokisaidia vyama vyao na jamii inayowazunguka.
Naye makamu mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika wa Kahawa wilayani Mbinga(Mbifacu)Erick Kinunda,ameipongeza Liyombo Amcos kwa kazi nzuri inayoleta matumaini makubwa kwenye sekta ya ushirika wilayani Mbinga.
“Liyombo Amcos imesaidia kuondoa dhana mbaya waliyonayo baadhi ya watu kufikiria kwamba kazi ya ushirika ni kukalia fedha,sisi kama Chama kikuu tutaendelea kuvisimamia vyama vya msingi(Amcos)kutimiza wajibu katika kuisaidia serikali yetu kuanzisha miradi mbalimbali ya maendeleo kama ilivyofanya Liyombo Amcos ambayo imejenga nyumba tatu ili kupunguza uhaba wa makazi kwa walimu wetu”alisema Kinunda
Muonekano wa nyumba bora ya walimu wa shule ya msingi Liyombo kata ya Linda Halmashauri ya Wilaya Mbinga iliyojengwa na Chama cha msingi cha Ushirika(Liyombo Amcos) ikiwa ni sehemu ya kupeleka faida kwa jamii.
