NA DENIS MLOWE, IRINGA
MBUNGE wa Jimbo la Iringa Mjini, Fadhili Ngajilo, ametoa onyo kali kwa mgambo wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kufuatia madai ya kuwanyanyasa wafanyabiashara wadogo maarufu kama machinga, akiwataka kusitisha mara moja vitendo hivyo.
Akiwa kwenye ziara ya kutembelea wamachinga katika Kata ya Miyomboni Kitanzini, Ngajilo alikutana na mamia ya wafanyabiashara wadogo na kupata fursa ya kusikiliza kero zao mbalimbali zinazowakabili katika shughuli zao za kila siku.
Akizungumza mbele ya umati huo, mwakilishi huyo wa wananchi alisema amekuwa akipokea malalamiko mengi yanayohusu ukamataji wa bidhaa, vipigo na vitisho vinavyodaiwa kufanywa na mgambo wa manispaa, hali inayosababisha hasara kubwa kwa wafanyabiashara.
Alisema kuwa wafanyabiashara wadogo ni nguzo muhimu katika uchumi wa mji na taifa kwa ujumla, kwani wanatoa ajira kwa vijana na akinamama pamoja na kuchangia kipato cha familia, hivyo hawastahili kufanyiwa ukatili katika jitihada zao za kujipatia riziki.
Ngajilo alieleza kuwa kupitia Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Iringa, maagizo tayari yametolewa kwa mgambo kuacha mara moja kuwanyanyasa machinga wakati taratibu bora za upangaji wa maeneo ya biashara zikiendelea kutafutwa.
Mbunge huyo alisema kuwa halmashauri inaangalia uwezekano wa kutenga maeneo maalum ya biashara pamoja na kuanzisha barabara mahsusi kwa ajili ya magulio ili kuhakikisha shughuli za ujasiriamali zinafanyika kwa mpangilio unaozingatia usalama na ustawi wa mji.
Aidha, alibainisha kuwa eneo la Mlandege linaendelea kuboreshwa ili kuendana na mahitaji ya wafanyabiashara na wateja wao, ikiwa ni sehemu ya mpango wa kuimarisha sekta isiyo rasmi ambayo imekuwa kimbilio kwa makundi mengi ya wananchi wanaojitafutia kipato.
Katika kuhimiza nidhamu, Ngajilo aliwataka machinga nao kufuata sheria na kanuni za mji kwa kujipanga vizuri, kuepuka kufanya biashara katika maeneo hatarishi au kuziba barabara ambazo hutumiwa na watembea kwa miguu na shughuli nyingine muhimu za jamii.
Mbunge huyo aliunga mkono msimamo wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan akisema haitaki kuona wananchi wake wakiteseka, na ndiyo maana inaendelea na mpango wa kujenga soko jipya la machinga katika eneo la Tembo Bar lililokuwa stendi ya zamani.
Kwa upande mwingine, Ngajilo alikemea tabia ya baadhi ya watu wanaojimilikisha maeneo ya wazi bila utaratibu na kuanza kuwatoza wengine fedha, akitaja mfano wa eneo lililoko nyuma ya Hoteli ya Babanusa, akisema hatua kali zitachukuliwa dhidi ya watakaobainika.
Wafanyabiashara walioshiriki mkutano huo walimshukuru Mbunge Ngajilo kwa kuwasikiliza na kuahidi kufuatilia suala hilo, wakisema kuwa kwa muda mrefu wamekuwa wakipoteza bidhaa na mitaji kutokana na kukimbizwa mara kwa mara na vitendo vya ukamataji visivyozingatia haki na utu.
