Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ilemela,Yusuf Bujiku, akifungua Mkutano wa Halmahauri Kuu ya CCM, wa kupokea utekelezaji wa Ilani, leo.
Na Baltazar Mashaka, Ilemela
MKUU wa Wilaya ya Ilemela, Amiri Mkalipa, amesema wilaya hiyo imepiga hatua kubwa za maendeleo baada ya kutekeleza miradi yenye thamani ya shilingi bilioni 58.423 zilizotokana na mapato ya ndani, serikali kuu na wadau wa maendeleo.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020–2025 katika Mkutano Mkuu wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Ilemela, uliofanyika katika ukumbi wa City Link, leo, Mkalipa alisema miradi hiyo imelenga kuboresha maisha na ustawi wa wananchi, mkutano uliohudhuriwa na wajumbe 102 kati ya 120.
Alisema katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2025, serikali imetekeleza miradi ya maendeleo katika sekta za elimu, afya, maji, utawala, barabara na umeme.
Kwa upande wa mapato ya ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, jumla ya shilingi bilioni 43.8 zilitumika katika sekta za afya na elimu, ikiwemo ujenzi na ukarabati wa miundombinu, ujenzi wa matundu ya vyoo shuleni pamoja na ununuzi wa mashine ya uchunguzi wa magonjwa katika Kituo cha Afya Buzuruga.
Katika sekta ya utawala, halmashauri ilinunua kangavuke (jenereta) la dharura kwa zaidi ya shilingi milioni 83, pikipiki kwa watendaji na maofisa maendeleo ya jamii, samani za ukumbi wa mikutano, kuboresha maegesho ya magari na kutoa mikopo ya uwezeshaji kwa makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Sekta ya maji kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) inatekeleza miradi yenye thamani ya shilingi bilioni 12.4. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 7.8 ni kwa ajili ya upembuzi yakinifu na usanifu wa mradi wa maji Kabangaja, unaotarajiwa kuzalisha lita milioni 200 kwa siku, kujenga matenki yenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni 50 na kusambaza maji kwa wananchi wapatao 800,000.
Mkalipa alisema kwa sasa uwezo wa uzalishaji maji ni lita milioni 138 kwa siku wakati mahitaji ni lita milioni 180, hivyo kuwepo upungufu wa lita milioni 42 unaosababisha mgawo wa maji, hivyo serikali inaendelea kutekeleza miradi ya matokeo ya haraka ili kuongeza uzalishaji na kukidhi mahitaji.
Aidha, shilingi bilioni 4.56 zimetengwa kwa miradi midogo ya matokeo ya haraka, ikiwemo ulazaji wa mabomba kutoka Buswelu Center hadi Ilalila kupokea maji kutoka Igoma Tenki. Mradi huo umefikia asilimia 98 na utanufaisha wananchi 51,123 wa Buswelu, Kahama Nyamadoke na Ilalila.
Mradi mwingine ni wa kuboresha mfumo wa usambazaji maji katika maeneo ya Bugogwa, Shibula, Nyafula, Igombe, Kayenze na Kilabela, wenye thamani ya shilingi milioni 294.8, ambapo kazi zitahusisha kuongeza mtandao wa mabomba kwa urefu wa kilomita mbili, ujenzi wa vituo vya kusukuma maji 22 na ununuzi wa pampu.
Katika sekta ya barabara, alisema licha ya juhudi za Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), bado changamoto ni ufinyu wa bajeti ya shilingi bilioni 2.706, huku miradi yenye thamani ya shilingi bilioni 1.22 ikiwa tayari imetekelezwa.
Kwa upande wa nishati, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limetumia shilingi milioni 470.152 kuunganisha umeme katika vitongoji 15, ambapo wananchi 2,743 kati ya 2,869 wameunganishiwa umeme kupitia mradi wa REA HEP II.
Katika mwaka wa fedha 2025/2026, shilingi 789,855,670.80 zimetengwa kwa ajili ya kupeleka na kuimarisha huduma ya umeme katika maeneo yenye miundombinu chakavu. Kati ya Julai mosi hadi Desemba 2025, zaidi ya shilingi milioni 400 zimetumika kupeleka umeme katika mitaa mbalimbali.
Mkalipa alisema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imeingia mkataba na kampuni ya QWIHAYA General Enterprises Co. Ltd kusambaza miundombinu ya umeme katika maeneo yaliyopimwa na ambayo hayajajengwa makazi, ili wananchi wabaki na jukumu la kuingiza umeme majumbani bila gharama za nguzo.
Alisema pia utekelezaji wa mradi wa Mission 300 (M300) wa miaka mitano utahakikisha upatikanaji wa miundombinu ya umeme katika maeneo yote yenye makazi.
Kwa upande wa mashirika yasiyo ya kiserikali, miradi 21 yenye thamani ya shilingi 472,646 imetekelezwa katika sekta za elimu, afya, uchumi, ulinzi na usalama wa mtoto pamoja na utunzaji wa mazingira, ikinufaisha wananchi 5,601 katika kata zote 19 za halmashauri.
Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ilemela, Yusuf Bujiku, alisema utekelezaji huo ni uthibitisho kuwa serikali ya CCM kuwa, imetekeleza kwa kiwango kikubwa miradi ya maendeleo katika kata zote za wilaya hiyo.
Alisema kutokana na mafanikio hayo, viongozi na wanachama wa CCM wana wajibu wa kuendelea kukijenga Chama kwa wananchi ili kudumisha imani na kuendeleza kasi ya maendeleo.sss

