Na Silivia Amandius.
Bukombe,Geita.
Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limesaini mkataba wa ushirikiano na kampuni ya uchimbaji madini ya Afrika Kusini ya Plantcor Mining and Plant Hire kwa ajili ya uchimbaji wa dhahabu katika leseni zake za Kigosi, wilayani Bukombe mkoani Geita February 23 mwaka huu.
Hafla hiyo ilishuhudiwa na Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, pamoja na viongozi wa Mkoa wa Geita na Wilaya ya Bukombe, ikionesha dhamira ya Serikali kuendeleza sekta ya madini kwa manufaa ya Taifa na wananchi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt. Venance Mwasse, alisema mkataba huo unalenga kuimarisha uzalishaji wa dhahabu kupitia ubia wa kimkakati, huku ukihusisha pia kufanya tafiti za anga (airborne survey) kwa kutumia ndege maalum ili kubaini taarifa sahihi za kijiolojia katika eneo lote la Kigosi.
Dkt. Mwasse alisisitiza kuwa mradi huo utaleta ajira na fursa za biashara kwa wazawa wa Bukombe na maeneo ya jirani, akiahidi kuwa STAMICO itatoa kipaumbele kwa wananchi wa eneo hilo kupitia sera ya Local Content.
Kwa upande wake, Dkt. Steven Kiruswa aliipongeza STAMICO kwa hatua hiyo na kuielekeza kuhakikisha mradi unazingatia utunzaji wa mazingira, uwajibikaji kwa jamii (CSR) na usimamizi wenye uwazi, huku akisisitiza kuwa jamii inayozunguka mradi lazima inufaike na rasilimali za eneo lao.
Naye Balozi Simon Sirro, Mwenyekiti wa Bodi ya STAMICO, alisema utiaji saini huo ni ishara ya kuimarika kwa mazingira ya uwekezaji nchini na kwamba ubia huo unatekelezwa kwa mujibu wa sheria huku maslahi ya wananchi yakilindwa.
Kwa upande wake, Josef Wilmans, Afisa Mtendaji wa Plantcor, alisema kampuni hiyo ina uzoefu wa zaidi ya miongo miwili katika shughuli za madini na imeleta utaalamu wa kiteknolojia na kifedha utakaosaidia kuongeza uzalishaji na ajira kwa Watanzania.
Aidha, Martin Shigella, Mkuu wa Mkoa wa Geita, aliahidi ushirikiano wa Serikali ya Mkoa ili kuhakikisha mradi unafanikiwa, huku Dkt. Dotto Mashaka Biteko, Mbunge wa Bukombe na Naibu Waziri Mkuu Mstaafu, akiwataka wananchi kuchangamkia fursa zitakazotokana na mradi huo ili kuharakisha maendeleo ya wilaya, mkoa na Taifa kwa ujumla.

