Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, Mariam Muhaj, amewataka waajiri na maafisa utumishi kuanza maandalizi ya watumishi wanaokaribia kustaafu angalau miaka mitano kabla ya muda wao kufika, ili kuwaepusha na changamoto za ucheleweshaji wa mafao.
Akifungua rasmi semina ya waajiri iliyoandaliwa na Public Service Social Security Fund (PSSSF) katika Ukumbi wa Hazina Ndogo mjini Babati Februari 23, 2026, Muhaj amesema changamoto za mifumo na kutokukamilika kwa taarifa zimekuwa kikwazo kwa wastaafu wengi kupata mafao yao kwa wakati.
Amesisitiza semina hiyo izingatie utoaji wa elimu ya matumizi sahihi ya mifumo ya kidijitali inayotumiwa na mfuko huo, huku akiwataka maafisa utumishi kufuatilia kwa karibu taarifa za watumishi wanaokaribia kustaafu ili kuhakikisha zinaendana na nyaraka husika.
Aidha, amewaagiza maafisa utumishi kuhakikisha madeni yote ya watumishi yanalipwa kabla ya kustaafu pamoja na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa mafaili ili kuondoa dosari zinazoweza kuchelewesha mafao.
“Serikali ni sikivu, lakini maafisa wanapaswa kutimiza wajibu wao mapema kwa kuwasilisha taarifa sahihi, inasikitisha kuona mtumishi anastaafu na kukaa muda mrefu bila mafao yake,” amesema Muhaj.
Kwa upande wake Meneja wa PSSSF, Kanda ya kaskazini ikijumuisha mikoa ya Arusha na Manyara, Yessaya Mwakifulefule, amesisitiza umuhimu wa waajiri na maafisa wanaoshughulikia wanachama wa mfuko huo kuwajibika ipasavyo ili kuhakikisha wastaafu wanapata mafao yao kwa haki na kwa wakati.
Amesema semina hiyo imelenga kutoa elimu kuhusu huduma za mfuko, kuimarisha ushirikiano kati ya PSSF na waajiri, pamoja na kuhakikisha malengo ya mfuko yanafikiwa.
Mwakifulefule ameonya kuwa uzembe wa maafisa unaweza kusababisha mateso yasiyo ya lazima kwa wastaafu, akibainisha kuwa uwajibikaji uliotukuka ni msingi wa kuwawezesha wastaafu kufurahia maisha baada ya utumishi.
Semina hiyo imehudhuriwa na maafisa utumishi pamoja na waajiri mbalimbali wa Mkoa wa Manyara, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuboresha huduma kwa wanachama na kuhakikisha wastaafu wananufaika haraka na mafao yao.

