Mwenyekiti wa Taifa wa chama cha ACT-Wazalendo, Othman Masoud Othman, ametimiza ahadi yake ya kuchangia mifuko 100 ya saruji kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Tawi la chama hicho katika eneo la Wingwi Mapofu (Mapofu A), Jimbo la Wingwi, Wilaya ya Micheweni.
Mifuko hiyo ya saruji imekabidhiwa kwa uongozi wa tawi hilo na Mwenyekiti wa Mkoa wa Micheweni, Rashid Khalid Salim, kwa niaba ya Mwenyekiti wa Taifa.
Akizungumza wakati wa makabidhiano, Rashid aliutaka uongozi wa tawi hilo kutumia mchango huo kama ulivyokusudiwa ili kumpa nafasi Mwenyekiti wao kuendelea kutoa michango zaidi siku zijazo.
Kwa upande wake, uongozi wa Tawi la Wingwi Mapofu (A) kupitia Mwenyekiti wa Ngome ya Wazee, Mbarouk Ali Mbarouk, aliyepokea msaada huo kwa niaba ya Mwenyekiti wa Tawi, ulisema unathamini mchango huo na umeahidi kumuandikia barua rasmi ya shukrani Mwenyekiti wa Taifa kwa msaada alioutoa.
Naye Katibu wa Jimbo la Wingwi kupitia ACT-Wazalendo, Abdallah Ali Said, aliwataka viongozi wa matawi mengine jimboni humo kuanza kujenga matawi yao ili kuimarisha utekelezaji wa shughuli za chama kwa ufanisi na kuchochea maendeleo ya chama kwa ujumla.
Mwenyekiti wa Taifa alikuwa ametoa ahadi hiyo wiki iliyopita wakati wa ziara maalum ya kukagua maendeleo ya chama na kuweka jiwe la msingi, na sasa ametimiza ahadi hiyo kwa vitendo

