Na John Bukuku – Dar es Salaam
Tume ya Ushindani nchini Fair Competition Commission (FCC) imewasilisha mfumo wake mpya wa kudhibiti bidhaa bandia kwa wahariri wa vyombo vya habari katika semina iliyofanyika leo mtaa wa Luthuli, Posta jijini Dar es Salaam, kati ya FCC na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF).
Akiwasilisha mada katika semina hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Kupambana na Bidhaa Bandia wa FCC, Salvator Gaspar Chuwa, amesema utekelezaji wa sheria unafanyika kwa kutumia mkakati wa kidijitali unaounganisha sheria na teknolojia ili kuzuia bidhaa bandia kuingia nchini.
“Utekelezaji wetu unategemea mfumo wa kidijitali unaotambua mizigo yenye vihatarishi kwa kutumia TANOGA, ambapo kibali cha forodha hutolewa tu baada ya ukaguzi na idhini ya FCC,” amesema Chuwa.
Ameeleza kuwa FCC imeanzisha Daftari la Kielektroniki la Alama za Biashara (Recorded Trademark Register) linalowezesha wakaguzi kuthibitisha papo kwa papo uhalali wa alama za biashara, nchi ya asili ya bidhaa pamoja na wazalishaji walioidhinishwa kabla ya bidhaa kuruhusiwa kuingia sokoni.
Kwa mujibu wa Chuwa, bidhaa zenye shaka huzuiliwa mara moja na Notisi za Ukamataji kutolewa, huku wahusika wakikabiliwa na adhabu ikiwemo faini, kutaifisha na kuharibu bidhaa bandia.
Akizungumzia hatua za uzingatiaji kwa wafanyabiashara, Chuwa amesema wamiliki wa alama za biashara wanatakiwa kuwasilisha maombi FCC pamoja na nyaraka husika, ambapo Mkaguzi Mkuu hupitia ndani ya siku 21 kabla ya kuidhinisha au kukataa, na alama zilizoidhinishwa huingizwa katika daftari rasmi.
Hata hivyo, amebainisha changamoto zinazoweza kujitokeza kuwa ni pamoja na uelewa mdogo kwa baadhi ya waagizaji na wafanyabiashara wadogo kuhusu mchakato wa recordation, utegemezi wa mifumo ya kidijitali pamoja na uwezekano wa wafanyabiashara haramu kutumia njia zisizo rasmi za mipakani.
“Mpango huu una faida kubwa kwa taifa. Unalinda usalama wa watumiaji, unaimarisha ushindani wa haki kwa biashara halali, unaongeza mapato ya serikali kwa kupunguza ukwepaji kodi na unaongeza imani kwa wawekezaji,” amesema Chuwa.
Ameongeza kuwa FCC inaendelea na utekelezaji wa miradi miwili mikubwa ya kidijitali ambayo ni Daftari la Kielektroniki la Alama za Biashara na Tovuti ya Maombi ya Alama za Biashara itakayorahisisha uwasilishaji, mapitio na uhuishaji wa maombi kwa njia ya mtandao.
Semina hiyo imelenga kuwajengea wahariri uelewa mpana kuhusu mfumo wa udhibiti wa bidhaa bandia ili kusaidia kuelimisha umma na kuimarisha mapambano dhidi ya biashara haramu nchini.

