Na.Sophia Kingimali.
Meneja wa Wakala wa Vipimo Mkoa wa Ilala, Muhono Nashon, amesema wakala umejipanga kuendelea kutoa elimu kwa wafanyabiashara kuhusu matumizi sahihi ya mizani na vipimo badala ya kutumia nguvu katika utekelezaji wa sheria.
Akizungumza katika kikao na wafanyabiashara wa Soko la Ilala jijini Dar es Salaam,leo Februari 20,2026 Nashon amesema elimu hiyo inalenga kujenga uelewa wa pamoja kabla ya maafisa wa vipimo kuanza ukaguzi mitaani.
Amesema wakala umejikita kutoa mafunzo kwa wafanyabiashara wanaotumia mizani ya aina mbalimbali ili kuhakikisha wanazingatia viwango vinavyotakiwa kisheria.
“Tunataka tunapokwenda kufanya ukaguzi tuwe tunaongea lugha moja na wafanyabiashara. Elimu ni muhimu kwa sababu wapo wapya sokoni na wengine hawafahamu taratibu za vipimo,” amesema.
Nashon ameongeza kuwa elimu haina mwisho, hasa katika mazingira ya masoko ambayo hupokea wafanyabiashara wapya mara kwa mara kwani baadhi ya changamoto hutokana na wafanyabiashara kutofahamu sheria, huku wengine wakifanya makosa kwa makusudi ili kujinufaisha.
Kwa upande wake, Katibu Msaidizi wa Soko la Ilala, Juma Bakari, ameiomba serikali kuhakikisha kunakuwa na usawa katika utekelezaji wa sheria za vipimo kuanzia mashambani hadi masokoni hivyo amesema si vyema wafanyabiashara kukamatwa sokoni pekee wakati changamoto zinaanzia katika maeneo ya uzalishaji.
“Ni muhimu elimu hii ikaenda hadi kwa wakulima mashambani. Pia vyombo vya habari vitumike kuelimisha umma ili kila mtu afahamu viwango vinavyotakiwa,” amesema Bakari, na akisisitiza kuwa hatua zisizo sawa zinaweza kuonekana kama kuna upendeleo au vitendo vya rushwa.
Nao baadhi ya wafanyabiashara wa jumla walieleza changamoto wanazokutana nazo wanaposafirisha mazao kutoka mikoa mbalimbali kwenda Dar es Salaam.
Wamesema mara kadhaa hulipa faini njiani na wanapofika sokoni hukumbana tena na adhabu kwa madai ya kuzidisha ujazo wa magunia.
Mfanyabiashara Stella Mwakamboje mfanyabiashara wa viazi amesema tofauti ya vifungashio kama “mfuto” au “rumbesa” katika mikoa kama Mbeya na Njombe huleta mkanganyiko wa bei na ushindani usio sawa sokoni.
Amesema hali hiyo huathiri uwezo wao wa kurejesha mikopo wanayochukua kuendesha biashara hivyo
Wafanyabiashara hao wameiomba serikali kuweka utaratibu mmoja wa kitaifa wa vifungashio na vipimo ili kuondoa tofauti hizo hivyo wamesisitiza kuwa iwapo mizani itatumika rasmi, basi iwe kwa wote kuanzia mashambani hadi masokoni ili kuleta usawa wa kibiashara.
Mwenyekiti wa Soko la Ilala, Ali Mbiku, ameipongeza Wakala wa Vipimo kwa kutoa elimu hiyo akisema itasaidia kulinda maslahi ya walaji na wafanyabiashara.
“Matumizi ya mizani yatasaidia mfanyabiashara kujua faida halisi badala ya kutegemea makadirio ya ujazo wa gunia”,Amesema.
Sambamba na hayo,Mbiku amelalamikia baadhi ya halmashauri kutoza faini kwa madai ya ukiukwaji wa vipimo wakati mamlaka ya kusimamia vipimo ipo kwa Wakala wa Vipimo pekee hivyo amesema ni muhimu mamlaka husika zishirikiane ili kuondoa migongano inayowaumiza wafanyabiashara.
Kwa ujumla, wadau wa soko hilo walikubaliana kuwa utoaji wa elimu endelevu na usimamizi wa pamoja wa sheria za vipimo utasaidia kuleta haki, uwazi na kuimarisha biashara katika masoko ya Jiji la Dar es Salaam na nchini kwa ujumla.

