Na. Meleka Kulwa- Fullshangwe Blog, Dodoma
Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Prof. Eliamani Sedoyeka, amesema kuwa chuo hicho kimejikita katika kuwaandaa vijana kwa kuwapatia elimu ya fedha na ujuzi wa biashara ili waweze kujiajiri na kujitegemea.
Akizungumza na waandishi wa habari Februari 20, 2026, katika ukumbi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma, Prof. Sedoyeka amesema vijana wengi wana ujuzi wa kitaaluma na kiufundi, lakini wanakosa maarifa ya namna ya kuugeuza ujuzi huo kuwa fursa ya ajira.
Amesema kuwa kila mwanafunzi anayepita chuoni hapo hupatiwa elimu ya fedha, huku kituo atamizi kikiwasaidia vijana kuchukua mawazo yao na kuyaandaa kitaalamu hadi kuwa mipango ya biashara inayoeleweka. Amesema baada ya hapo, vijana huendelea na masomo ya biashara kwa ujumla pamoja na elimu ya fedha na nidhamu ya matumizi, ikiwemo namna ya kupata fedha kupitia maandiko yao ya biashara.
Aidha amebainisha kuwa chuo huwapa vijana hamasa ya kuanza na rasilimali walizonazo, huku wale wenye nia ya dhati wakianza kwa kubaini kiwango cha mtaji wanaohitaji.
Amesema wapo vijana wanaoanza kwa shughuli ndogo kama kupika uji asubuhi, kuuza kwa wenzao kwa kutumia thermos na kuwaajiri vijana wengine, hali inayowezesha biashara kukua hadi kupewa duka ndani ya chuo kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao.
Pia ameongeza kuwa katika kuimarisha ajira kwa vijana, chuo kimeanzisha mtaala mpya wa uhasibu na kodi unaolenga kumwezesha kijana kujiajiri.
Amesema wahitimu wanaweza kusaidia biashara ndogo na za kati kuandaa hesabu, kuziweka vizuri na kutengeneza taarifa za kodi. Ameongeza kuwa mtaala wa Accountancy International unawaunganisha vijana na ujuzi na weledi unaowawezesha kuingia kwenye soko la ajira au kujiajiri.
Prof. Sedoyeka amesema kuwa Serikali imeendelea kuwekeza katika chuo hicho kwa lengo la kuwafikia wananchi zaidi, huku asilimia 90 ya wanafunzi wakiwa vijana wa wastani wa umri wa miaka 20.
Aidha, Amesema kuwa kozi zinazotolewa zimeandaliwa kwa kuzingatia uhalisia wa mahitaji ya vijana na soko la ajira, Aidha amebainisha kuwa chuo kina ushirikiano na Jeshi la Magereza katika kuwapatia vijana walioko gerezani na wanaokaribia kutoka mafunzo ya elimu ya fedha na ujuzi wa kujiajiri, ili wanapotoka waweze kuanza shughuli halali na kuepuka kurejea tena gerezani. Amesema mafunzo hayo hutolewa kidigitali kutoka chuoni hadi gerezani.
Pia ameongeza kuwa chuo kinatarajia kushirikiana na Wizara ya Elimu ili kuona namna ya kuchangia katika kufundisha walimu au kutoa mafunzo moja kwa moja kwa lengo la kuziba pengo la elimu kwa vijana.
Aidha, amebainisha kuwa chuo kina wanafunzi 20,993 katika kampasi zake mbalimbali, huku takribani wanafunzi 1,000 wakiwa siyo active kutokana na changamoto mbalimbali. Aidha, kila mwaka hupokea wanafunzi 30 hadi 40 wa Shahada ya Uzamili, wengi wao wakiwa vijana wanaofanya kazi katika mashirika ya kimataifa, balozi au wanaoishi nje ya nchi.
Amesema gharama za kusoma Shahada ya Uzamili nje ya nchi hufikia kati ya shilingi milioni 100 hadi 200, wakati wanaosoma ndani ya nchi hulipa takribani shilingi milioni nne.

