Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Nyasa Mkoani Ruvuma Khalid Khalif,akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi na shughuli mbalimbali za maendeleo zilizotekelezwa kwa mwaka wa fedha 2025/2026 wakati wa kikao cha  Baraza la Madiwani kwa mwaka wa fedha 2026/2027 kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri hiyo jana ambapo zaidi ya Sh.bilioni 33.2 zimepangwa kukusanywa kutoka vyanzo  mbalimbali vya mapato.

Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya Nyasa,wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya hiyo  Peres Magiri (hayupo pichani) wakati wa kikao cha robo ya pili cha Baraza la Madiwani kwa mwaka wa fedha 2026/2027 kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri hiyo jana.

Baadhi ya wakuu wa idara na vitengo wa Halmashauri ya Wilaya Nyasa Mkoani Ruvuma, wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya hiyo Peres Magiri(hayupo Pichani) wakati wa kikao cha robo ya pil cha Baraza la Madiwani kwa mwaka wa fedha 2026/2027 kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri hiyo eneo la Kilosa ambapo Baraza hilo lilipiptisha rasimu ya bajeti ya Sh.bilioni 33.2.

Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Mkoani Ruvuma Peres Magiri,akitoa salamu  za Serikali wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wlaya hiyo jana  ambao amewataka Madiwani kwenda kusimamia suala la mapato ya ndani na kushiriki kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Mbunge wa Jimbo la Nyasa John Nchimbi,akizungumza  na Madiwani na watumishi(hawapo pichani)  wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya Nyasa  cha kujadili  na kupitisha rasimu ya mpango wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2026/2027,Halmashauri ya Wilaya Nyasa imepitisha  zaidi ya Sh.bilioni 33.2 kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo.

…………..

Na Mwandishi Maalum, Nyasa

BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya Nyasa Mkoani Ruvuma,limepitisha rasimu ya mpango  wa Bajeti kwa mwaka wa fedha 2026/2027 ambapo kiasi cha Sh.33,254,317,000.00 zimepangwa kukusanywa kwa ajili ya kutekeleza shughuli mbalimbali ikiwemo ujenzi wa miradi ya maendeleo.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Khalid Khalif,kwenye kikao cha robo ya pili cha Baraza la Madiwani kwa mwaka wa fedha 2026/2027 kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri hiyo eneo la Kilosa.

Khalif alisema,kati ya fedha hizo Sh.20,118,640,000.00 kwa ajili ya mishahara wa watumishi sh.1,441,049,000.00 za matumizi mengineyo, Sh.8,433,099,000.00  zitatumika kutekeleza miradi ya maendeleo na Sh. 4,305,638,000.00 ni fedha za ndani huku Sh.4,127,461,000.00 ni fedha za maendeleo ya nje.

Khalif alisema,Sh.3,261,529,000.00 fedha za mapato ya ndani Sh.2,039,267,000.00 fedha za mapato ya ndani halisia, Sh.1,222,262,000.00 mapato lindwa na Sh.437,853,400.00 fedha za mapato ya ndani kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Kwa mujibu wa Khalif, sehemu kubwa ya bajeti  ya mwaka  wa fedha 2026/2027 imelenga zaidi kuchochea maendeleo,kuboresha huduma za jamii na ustawi wa wananchi wa Wilaya ya Nyasa.

Amewataka madiwani kuendelea kushauri na kutoa maoni kwa njia zilizo rasmi  kwa ajili ya uboreshaji na uendeshaji wa majukumu ya kila siku ya Halmashauri na kushirikiana na watumishi ili kuleta mafanikio.

Mbunge wa Jimbo la Nyasa John Nchimbi,amewataka madiwani kuwa na umoja kwenye majukumu yao hatua itakayosaidia kuijenga Halmashauri yao.

“Bajeti hii ni muhimu sana kwa ajili ya maendeleo ya wilaya yetu,twendeni tukakamilishe miradi iliyosimama ambayo ilipaswa kukamilika mwaka wa fedha uliopita ambayo fedha zake bado zipo na hazijatumika”alisema Nchimbi.

Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Pers Magiri,amewataka madiwani kuhakikisha wanajielekeza kujua na kutimiza wajibu wao na kuwasaidia wananchi badala ya kutanguliza maslahi  yao binafsi.

“Naona robo tatu ya madiwani wa zamani leo hawapo katika Baraza hili,nawaomba sana nyinyi mliobaki na  madiwani wapya mkatumie muda wenu kuwatumikia wananchi na kutekeleza shughuli za maendeleo kwa kushirikiana na wananchi wenu,mapato ya ndani yanatoka kwenu na uendeshaji wa Halmashauri sehemu kubwa inategemea mapato ya ndani na sio vinginevyo”alisema Magiri.

Aidha Magiri, amewataka wataalam kusimama kwenye majukumu yao na madiwani wana wajibu wa kufuatilia utekelezaji wa miradi yote katika kata zao badala ya kuwaachia watendaji wa Serikali,kwani wao ni sehemu ya miradi hiyo.

“Ndugu zangu madiwani naowamba sana tusijiingize kufanya kazi za ujenzi ya miradi inayoletwa kwenye kata zenu ili kuepuka kuwa sehemu ya matatizo,sikatazi diwani kufanya kazi lakini ni lazima awe na sifa inayotakiwa”alisisitiza Dc Magiri.

Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Piniel Mbura alisema Wilaya ya Nyasa imeendelea kufanya vizuri kimapato kutoka wastani wa Sh.bilioni 2.4 mwaka wa fedha 2024/2025 hadi kufikia Sh.bilioni 3.2 mwaka wa fedha 2026/2027.

Mbura,amewataka madiwani kuacha kuzalisha migogoro inayoweza kurudisha nyuma jitihada zinazofanywa na watumishi za  kuharakisha maendeleo katika Halmashauri yao bali wawe chachu ya mafanikio.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Nyasa Stewart Nombo,amewasisitiza wataalam kuongeza juhudi katika kusimamia miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwenye maeneo yao,kuepuka kuingilia majukumu mengine ya kiutendaji.