Na Silivia Amandius, Kagera.
Wakala wa Nishati Vijijini (REA) mkoani Kagera umetambulisha rasmi mradi mkubwa wa upelekaji umeme katika vitongoji 474, hatua inayolenga kuongeza upatikanaji wa nishati vijijini na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Mradi huo unatekelezwa na mkandarasi CCC International Engineering Nigeria Ltd.
Kwa mujibu wa Meneja Miradi Kanda ya Ziwa, Mhandisi Ernest Makale, jumla ya kilomita 737.3 za njia ya umeme wa msongo wa kati (MV) na kilomita 768 za msongo mdogo (LV) zinajengwa, pamoja na ufungaji wa transfoma 474 ambapo Zaidi ya shilingi bilioni 66 zinatarajiwa kutumika katika utekelezaji wa mradi huo ambao utaunganisha wateja 15,396 katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Kagera na utatumia miezi 36 kukamilika Kwa mradi huo.
Wilaya zitakazonufaika na mradi huo ni Ngara, Biharamulo, Muleba, Bukoba Vijijini, Missenyi, Karagwe na Kyerwa. Kila wilaya imepangiwa idadi tofauti ya vitongoji kulingana na mahitaji na hali ya miundombinu iliyopo, huku lengo kuu likiwa ni kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata huduma ya umeme na kuboresha maisha yao.
Mradi huo unafadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Dunia. Utekelezaji wake unatarajiwa kuongeza fursa za ajira, kukuza biashara ndogo na za kati, kuboresha huduma za elimu na afya, pamoja na kuinua uchumi wa wananchi kwa ujumla.
Akizungumza wakati wa utambulisho wa mradi huo katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mkuu wa Mkoa, Kanali Yahya Ramadhan Kido, amewataka wataalamu kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa ufanisi na kukamilika kwa wakati huku akisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imelenga kuwasogezea wananchi huduma muhimu karibu yao, hivyo changamoto zozote zitakazojitokeza ziwasilishwe mapema katika ofisi yake kwa ajili ya ufumbuzi wa haraka.
Licha ya hayo amewahimiza wakandarasi na wataalamu kutoa taarifa kwa viongozi wa vijiji wanapofika maeneo ya utekelezaji ili kupata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa wananchi na kusema malengo ya mradi huo kuwa ni pamoja na kutoa ajira kwa vijana na wanawake, kuchochea shughuli za uzalishaji mali na kuleta mabadiliko chanya katika maisha ya wakazi wa Mkoa wa Kagera.

