Ashrack Miraji Fullshangwe Media 

Mbunge wa Jimbo la Vunjo Enock Koola* na Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini Morris Makoi kwa pamoja wameamua kushirikiana ili kuweza kupandisha uzalishaji mkubwa wa zao la Kahawa katika Wilaya ya Moshi. 

Hatua hiyo imekuja baada ya kuanda kikao maalumu kinachohusisha wadau mbalimbali kutoka majimbo yote mawili ambao ni vyama vya Ushirika, TACRI, Bodi ya Kagawa Tanzania (TCB), APK, KPL, Afisa kilimo wa Wilaya na Afisa Ushirika wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi.

Katika kikao hicho Enock Koola Mbunge Jimbo la Vunjo alieleza lengo la serikali na mpango wa serikali kuongeza nguvu kwenye zao la kimkakati la kahawa, na mpango wa serikali wakuhakikisha zaidi ya tani laki tatu kwa mwaka zinazalishwa. 

Mbunge alisema “Ni masikitiko makubwa sana kuona wilaya yetu ya Moshi kwa ujumla inazalisha tani elfu moja tu kwasasa huku malengo ya Serikali ni kuzalisha tani laki tatu kwa mwaka. Ikizingatiwa Mkoa wa Kilimanjaro ndio zao la msingi kabisa kwa historia na uzalishaji wake”.

Mbunge Koola, amewataka wadau kutoa mawazo yao namna gani ya kuboresha uzalishaji mkubwa wa zao la kahawa ambalo hapo awali lilikuwa tegemeo na baadae kuporomoka bei hivyo kupelekea wakulima wengi kukakata tamaa na kuacha kuendelea kulima.

Kwa upande wa Moriss Makoi Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini aliwahakikishia wadau tayari Bilioni 3 zimepatikana kutoka serikalini kwa ajili ya kuboresha mfereji wa Makeresho. 

Mbunge* alisema, “naomba niwahakikishie serikali imepanga kuleta shilingi Bilioni 3 kwa ajili ya kuboresha mfereji wa maji wa Makeresho hivyo utasaidia sana katika shughuli nzima za umwagiliaji. Pia, aliwaomba KPL kusaidia wakulima wadogo wa kahawa ili wawe na uwezo wa kuzalisha kahawa nyingi”.

Aliongeza “Kwa jitihada zangu binafsi na kwa kushirikiana na Mbunge mwenzangu wa Jimbo la Vunjo tumenunua mitambo itakayosaidia sana kurekebisha Barabara zetu ziweze kupitika msimu mzima hivyo itasaidia Barabara za mashambani kufikika kwa urahisi na kuongeza uzalisha wa zao la kahawa”.