Na Silivia Amandius 

Bukoba.

Serikali ya Tanzania imeendelea kuwekeza kwa nguvu katika elimu ya ufundi stadi, ikiwa ni hatua ya kuhakikisha vijana wanapata ujuzi unaohitajika katika soko la ajira na kujiajiri, huku kila wilaya ikilengwa kwa njia ya vyuo vya VETA.

Akizungumza katika Chuo cha Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Kagera wakati wa ziara ya wajumbe wa Inter-University Council for East Africa (IUCEA) kutoka nchi nane, Mkurugenzi wa Mafunzo wa VETA, Dkt. Abdallah Ngodu, alisema Serikali inalenga kuhakikisha vijana wasiopungua 120,000 wanahitimu mafunzo ya ufundi stadi kila mwaka.

Dkt. Ngodu alisema kuwa mwaka uliopita, jumla ya vijana 86,000 walihitimu kutoka vyuo vya VETA kote nchini, hatua inayodhihirisha ukuaji mkubwa wa sekta ya ufundi stadi. Hadi sasa, Tanzania ina takribani vyuo 80 vya VETA vinavyotoa mafunzo, huku vyuo vingine 65 vikiwa katika hatua mbalimbali za ujenzi, na lengo ni kuhakikisha kila wilaya inakuwa na angalau chuo kimoja cha VETA ili huduma za ufundi stadi ziwe karibu na wananchi.

“Serikali ina dhamira ya kuhakikisha elimu ya ufundi stadi inawafikia wananchi wote bila ubaguzi. VETA inatoa nafasi kwa jinsia zote pamoja na makundi maalumu ili kila Mtanzania aweze kushiriki katika ujenzi wa uchumi wa nchi,” alisema Dkt. Ngodu.

Dkt. Ngodu pia alisema ziara ya wajumbe wa IUCEA ililenga kujionea uwekezaji mkubwa uliofanywa na Tanzania katika sekta ya ufundi stadi na kubadilishana uzoefu wa namna bora ya kukuza ujuzi kwa vijana wa Afrika Mashariki.

Kwa upande wake, Mratibu wa Kanda ya Afrika wa IUCEA, Dkt. Cosma Chawana Joseph, alisema nchi nyingi za Afrika zinaongeza uwekezaji katika ufundi stadi kwa kuwa ndiyo njia kuu ya kujenga ujuzi, maarifa mapya, na nguvu kazi ya vijana.

“Nchi za Afrika zinaendelea kushirikiana katika kuboresha elimu ya ufundi stadi. Hakuna ushindani, bali tunalenga kudumisha ushirikiano imara kwa maendeleo ya pamoja ya bara letu,” alisema Dkt. Chawana, akisisitiza kuwa Tanzania ni mfano wa uwekezaji mkubwa katika vyuo vya ufundi stadi, hususan vyuo vikubwa vinavyotoa mafunzo ya vitendo.