Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba, Dkt. Amon Mkoga, ametembelea Hospitali ya Wilaya ya Kwimba kwa lengo la kusikiliza kero za wananchi na kukagua huduma mbalimbali za afya zinazotolewa hospitalini hapo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha utoaji wa huduma kwa jamii.

Akizungumza na wananchi waliokuwa wakipatiwa huduma hospitalini hapo, Mkoga amesema ziara hiyo imelenga kupata mrejesho wa moja kwa moja kutoka kwa wananchi ili kubaini changamoto zilizopo na kuzitafutia ufumbuzi wa haraka.

“Ni wajibu wetu kama viongozi kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya. Nimefika hapa kusikiliza kero zenu na kuhakikisha tunazifanyia kazi kwa wakati,” amesema Mkoga.

Katika ukaguzi wake, ametembelea wodi ya wazazi, wodi ya watoto, maabara pamoja na kitengo cha wagonjwa wa nje (OPD), ambapo amewataka wataalamu wa afya kutoa huduma kwa weledi na kuzingatia maadili ya taaluma zao.

Kwa upande wake, Daktari Lunala Zengo amemuomba Mkurugenzi kuongeza jengo maalum la kujifungulia kwa wanawake wajawazito ili kupunguza msongamano na kuboresha huduma za uzazi hospitalini hapo.

Daktari huyo amesema ongezeko la wanawake wanaofika kujifungua hospitalini limekuwa kubwa, hivyo uhitaji wa jengo la kisasa lenye vifaa tiba vya kutosha ni muhimu katika kuhakikisha usalama wa mama na mtoto.

“Tunaomba mpango wa kuongeza jengo la wazazi ufanyike ili tuondoe msongamano na tuweze kutoa huduma katika mazingira bora zaidi kwa wazazi na watoto,” amesema Dkt. Zengo.

Ziara hiyo inaonesha dhamira ya Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba ya kusimamia kwa karibu utoaji wa huduma za afya na kuhakikisha wananchi wanapata huduma stahiki kwa wakati na kwa ubora.