…………
Na Happy Lazaro, Arusha .
HALMASHAURI ya Jiji la Arusha inahitaji kiasi cha shilingi bilioni 1.8 kwa ajili ya kurejesha miundombinu ya umma iliyoharibiwa katika vurugu za uchaguzi na baada ya uchaguzi, zilizosababisha kuchomwa kwa majengo ya serikali na kuathiri moja kwa moja utoaji wa huduma katika ngazi za kata na mitaa.
Hayo yameelezwa  leo kwenye kikao cha baraza la madiwani   na Diwani wa Kata ya Baraa, Jacob Meja, aliyetaka kujua ratiba ya kurejesha miundombinu hiyo na hatua za haraka za kurejesha utendaji wa ofisi zilizoathirika.
“Wakati matukio haya yakitokea, bajeti ya halmashauri ilikuwa tayari imepitishwa. Hivyo, tunaliomba Baraza la Madiwani kuidhinisha ombi la fedha katika bajeti ya mwaka wa fedha 2026/27 ili ukarabati ufanyike kwa wakati na huduma zirejee katika hali ya kawaida,” amesema Dkt. Maduhu.
Kwa mujibu wa taarifa ya uongozi wa jiji, uharibifu huo umeathiri shughuli za kiutawala na utoaji wa huduma za msingi ikiwemo usajili wa wakazi, uratibu wa miradi ya maendeleo ya mitaa, pamoja na ukusanyaji wa mapato ya ndani. Baadhi ya ofisi zimekuwa zikitoa huduma kwa muda kwa kutumia maeneo mbadala yasiyo na miundombinu stahiki.
“Baada ya uharibifu wa vurugu za uchaguzi oktoba 29,2026 Tathimini ya kwanza iliyofanyika katika maeneo yote ya mitaa na kata kiasi cha sh bilioni 1.866 zinahitajika “amefafanua  Dkt Maduhu.
Baraza la Madiwani linatarajiwa kujadili na kuidhinisha ombi hilo katika mchakato wa bajeti ijayo, hatua itakayofungua njia ya ukarabati wa majengo, ununuzi wa vifaa na kurejesha utendaji kamili wa ofisi za serikali za mitaa.
Wadau wa maendeleo na viongozi wa kijamii jijini humo wameitaka halmashauri, sambamba na ukarabati, kuweka mikakati madhubuti ya ulinzi wa miundombinu ya umma na kuimarisha mifumo ya tahadhari ili kuepusha madhara yanayoweza kuzuilika siku zijazo.