Mkurugenzi  Mkuu wa Tume ya TEHAMA (ICT Commission – ICTC) Dkt. Nkundwe Mwasaga, akizungumza na waandishi wa habari leo, Februari 12, 2026, jijini Dar es Salaam.

…………

NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM

Tume ya TEHAMA (ICT Commission – ICTC) imeanza kusajili na kutambua kampuni changa za TEHAMA, ambapo hadi kufikia mwezi Desemba 2025, zaidi ya kampuni changa 400 zilizo katika hatua mbalimbali za ukuaji na ubunifu, utoaji wa huduma zilisajiliwa, huku kaati ya hizo, kampuni 161 zimekidhi vigezo vya kuingia katika programu mbalimbali za uendelezaji na uwezeshaji katika maeneo tofauti, ikiwemo kitaalamu na rasilimali.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Februari 12, 2026, jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt. Nkundwe Mwasaga, amesema kuwa usajili huo haukuwa na gharama yoyote kwa kampuni changa na ulilenga kutambua mahitaji yao pamoja na bunifu za TEHAMA, ili kuwezesha upatikanaji wa rasilimali fedha au huduma za kitaalamu kutoka ndani na nje ya Serikali.

Dkt. Mwasaga amesema hatua hiyo itawezesha kampuni changa za TEHAMA kuingia sokoni na kukuza mitaji yao.

Aidha, itawezesha ICTC kutambua changamoto zinazozikabili kampuni hizo na kushirikiana na wadau mbalimbali kuanzisha jitihada za ujenzi wa miundombinu wezeshi, kutafuta na kutoa mafunzo ya kitaalamu ya biashara na ujasiriamali kwa kampuni zilizo katika hatua ya awali ya ukuaji (early stage), pamoja na kuwezesha upatikanaji wa mitaji kwa kampuni zilizo katika hatua ya ukuaji (growth stage).

“Mpango huu wa utambuzi wa kampuni changa za TEHAMA unalenga kuongeza ufanisi wa uwezeshaji katika kufikia vigezo vya nafuu za uwekezaji, ugavi na manunuzi ya umma, pamoja na nafuu za leseni za udhibiti chini ya mamlaka mbalimbali zinazotolewa na Serikali kupitia taasisi zake kwa mujibu wa sheria,” amesema Dkt. Mwasaga.

Amesema mpango huo pia utasaidia kujenga imani kwa wadau wa ndani na nje ya nchi ili kuwapatia fursa kampuni changa za TEHAMA za Tanzania kufanya majaribio ya matumizi ya bidhaa na huduma walizobuni, kama hatua ya awali ya kuingia katika soko la biashara, kuwekeza au kuingia makubaliano ya kibiashara.

Dkt. Mwasaga amesema mpango huo utaongeza ufanisi wa programu maalum za kuzitangaza kampuni changa za TEHAMA kwa wawekezaji na masoko mbalimbali kupitia mikutano mikubwa ya kibiashara na kiserikali inayofanyika ndani na nje ya nchi, pamoja na kupitia makubaliano ya kidiplomasia ya uwili (bilateral) na uwingi (multilateral) kati ya Tanzania na nchi nyingine.

“Itakuza programu za kujenga uwezo kwa kampuni changa za TEHAMA katika nyanja za biashara, masoko, kodi, TEHAMA na haki miliki, kwa kushirikiana na wadau wa ndani na nje ya nchi,” amesema Dkt. Mwasaga.

Amefafanua kuwa utaratibu huo umefanyiwa tafiti katika nchi mbalimbali zilizopiga hatua kubwa katika uwezeshaji wa kampuni changa ndani na nje ya Afrika, ikiwemo Estonia, India, Algeria na Tunisia.
Aidha, ametoa wito kwa kampuni changa yoyote ya TEHAMA kujisajili na kupata utambuzi maalum unaotolewa na Tume ya TEHAMA, ili iweze kutambuliwa na kuingizwa katika programu mbalimbali za uwezeshaji.

Mchakato wa usajili na utambuzi hauna gharama yoyote kwa kampuni changa za TEHAMA. ICTC itakuwa ikitoa orodha ya kampuni zilizojisajili na kupewa utambulisho maalum kila baada ya miezi mitatu. Orodha ya kwanza ya kampuni zilizojisajili hadi Desemba 2025 itatolewa wakati wowote mwezi huu wa Februari 2026, baada ya kukamilika kwa hatua za mwisho za uchambuzi.