Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM Mkoa wa Mwanza, Mohamed Lukonge, akizungumza na wajumbe wa kikao cha kawaida cha jumuiya hiyo (hawapo pichani), leo.

Na. Baltazar Mashaka – Mwanza

JUMUIYA ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mwanza, imehimizwa umuhimu wa malezi bora kwa vijana kuwa, ni nyenzo ya msingi ya kutunza maadili, kuhakikisha usalama na maendeleo ya jamii ili kuimarisha ustawi wa taifa.

 

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Michael Masanja ‘Smart’, alitoa kauli hiyo leo, alipofungua kikao cha kawaida cha Jumuiya hiyo katika ukumbi wa Maji House, ili kuzungumzia maendeleo na kuchambua changamoto za kijamii na kisiasa zilizojitokeza baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.

 

Akizungumza na wajumbe wa jumuiya hiyo, Smart alisema, Jumuiya ya Wazazi ina kazi kubwa ya kuongoza mchakato wa malezi na utunzaji wa vijana, kuhakikisha wanawalea katika maadili mema na kuwa raia wema wenye kuunga mkono misingi ya amani, utulivu na maendeleo endelevu.

 

“Wazazi ni nguzo muhimu ya jamii. Tunapaswa kuhakikisha vijana wetu wanakuwa na maadili mema ambayo yatakuwa msaada kwao binafsi na kwa taifa kwa ujumla, katika mustakabali wa kujenga kizazi na taifa lenye maadili bora,” alisema Smart.

 

Alisema kuwa, changamoto zilizojitokeza katika baadhi ya maeneo Oktoba 29, 2025 zilitokana na ukosefu wa malezi bora na upungufu wa msukumo wa maadili katika familia na jamii, jambo lililochochea vurugu na migogoro isiyokuwa ya lazima.

 

“Mnayo kazi kubwa ya malezi ya vijana.Yaliyotokea Oktoba 29, 2025, yalitokana na vijana kukengeuka maadili ya Kitanzania, hivyo mna kazi ya kuwalea katika maadili mema kwa maslahi ya Chama, jamii na taifa,”alisema Mwenyekiti huyo wa CCM Mkoa wa Mwanza.  

 

Pia, Smart aliipongeza Jumuiya ya Wazazi kwa mchango wake katika kuhakikisha ushindi wa CCM katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 na kwa michango yao mbali mbali ikiwemo kuwahamasisha wanachama kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kisiasa.

 

Aidha, alisisitiza kuwa Jumuiya ya Wazazi ni moja ya nguzo muhimu za CCM kuanzia ngazi ya shina hadi taifa, inalenga siyo tu malezi ya vijana bali pia utunzaji wa mazingira, elimu na maendeleo ya jamii kwa ujumla.

Aliiwashukuru wajumbe Jumuiya hiyo ya Wazazi kwa kuanzisha na kuendeleza shule ya Sekondari Kahunda ambayo imekuwa ikitoa fursa ya elimu kwa vijana wa mkoa huo na maeneo mengine.

Jumuiya ya Wazazi, iliyotimiza miaka 48 tangu kuanzishwa kwake 1955, awali ilijulikana kama TAPA, kabla ya kubadilika jina 1978), imekuwa ikifanya shughuli mbalimbali za kijamii na kisiasa ndani ya CCM.

Smart aliwaeleza wajumbe wa kikao hicho kuwa, anaamini kitakuwa chenye mafanikio yenye tija na kitatoa mwanga na mwelekeo kwa mikakati ya baadaye ya kuimarisha malezi na elimu ya maadili kwa vijana kwa maslahi ya jamii na CCM.

Awali, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Mwanza, Mohamed Lukonge, alisema kikao hicho kilipaswa kufanyika Desemba 2025, kilikuwa fursa muhimu ya kujadili nyanja mbalimbali za maendeleo ya jumuiya, malezi, utunzaji wa mazingira na kuimarisha mshikamano miongoni mwa wajumbe.

Alitoa pongezi kwa wajumbe kwa kazi yao kubwa ya kampeni na ushiriki katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana, na kuwezesha CCM kupata ushindi mkubwa wa kishindo , akawataka kuendelea kuwa nguzo thabiti ya Chama na jamii kwa ujumla.