Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Camillus Wambura, akiwa ameambatana na Kamishna wa Fedha na Lojistiki CP Liberatus Sabas pamoja na maafisa wengine amefanya ukaguzi wa maendeleo ya Mradi wa Ujenzi wa nyumba za Wakufunzi na Familia zao na Mabweni ya Wanafunzi katika shule ya Polisi Moshi Mkoani Kilimanjaro.

Ujenzi huo unatekelezwa na Serikali ya awamu ya sita chini ya Amiri Jeshi Mkuu Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwezesha na kuboresha upatikanaji wa miundombinu ya majenzi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa ndani ya Jeshi la Polisi.

Itakapo kamilika miradi hiyo katika Shule hiyo ya Polisi Moshi utawaongezea morali katika utendaji kazi sambamba na kukuza ustawi wa askari kwa kukaa na kuishi kwenye mazingira bora na ya kisasa jambo litakalo wawezesha kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi.

Mbali na uboreshaji huo wa miundombinu ya makazi ya wakufunzi na wanafunzi upo uboreshaji wa mitaala ambao umefanyika sambamba na kuingia kwenye mikataba na vyuo vya ndani ya nchi ili kuendana na utekelezaji wa Mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai iliyopendekeza Askari kujengewa uwezo ambapo imewezesha Maafisa, Wakaguzi na Askari 111 kufanikiwa kuhitimu masomo katika kiwango cha Uzamili (Masters) kwa mwaka 2025 kutokana na uwepo wa Tawi la IAA (Institute of Accountancy Arusha) katika Shule hiyo ya Polisi Moshi ambao wanaendesha kozi mbalimbali za kuwajengea uwezo na ujuzi Askari kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi.