Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya (MZRH) imeendelea kuandika historia mpya katika sekta ya afya baada ya kusaini makubaliano ya ushirikiano na Shirika la CURE Neuro lenye makao makuu Michigan, Marekani. Ushirikiano huo unalenga kuimarisha huduma za matibabu kwa watoto wenye tatizo la vichwa kujaa maji (Hydrocephalus) na mgongo wazi (Spina Bifida), huku ukaiweka hospitali hiyo katika ramani ya kimataifa ya utoaji wa huduma za kibingwa.

Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini wa makubaliano hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya, Dkt. Godlove Mbwanji, amesema dira ya hospitali ni kuwa kituo kinara cha utoaji wa huduma za kibingwa na kibobezi zenye viwango vya kimataifa. Ameishukuru CURE Neuro kwa utayari wake wa kushirikiana na Tanzania kuhakikisha wananchi wa ndani na kutoka nchi jirani wenye changamoto hizo wanapatiwa matibabu bora na salama bila ubaguzi.

Kupitia makubaliano hayo, hospitali itanufaika na matumizi ya teknolojia na vifaa vya kisasa vya upasuaji vinavyotumika katika hospitali za kimataifa, ikiwemo hospitali maalum ya watoto inayoshughulika na matatizo ya ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu ya CURE Neuro iliyopo Mbale, Uganda, iliyo chini ya shirika hilo. Hatua hii itaongeza ubora, usalama na ufanisi wa huduma kwa watoto wa Tanzania na nchi jirani bila kulazimika kusafiri umbali mrefu kutafuta matibabu, sambamba na kujenga uwezo wa wataalamu kupitia mafunzo na kubadilishana uzoefu na wataalamu wa kimataifa.

Naye Meneja wa Mradi wa CURE Neuro chini ya CURE International (Africa Division), Joshua Menya, ameishukuru Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya kwa kukubali kushirikiana nao, akieleza kuwa makubaliano hayo yatafungua ukurasa mpya wa huduma za kibingwa. Amebainisha kuwa CURE Neuro ina imani kubwa na uwezo wa wataalamu wa hospitali hiyo, na kwamba kwa pamoja watahakikisha watoto wengi zaidi wanapata huduma bora kwa wakati.

Mbali na kuboresha huduma kwa wananchi wa Tanzania, hatua hiyo pia imefungua ukurasa mpya wa ukuaji wa utalii wa matibabu (medical tourism) katika Ukanda wa Nyanda za Juu Kusini.