Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Mbinga Mkoani Ruvuma Joseph Kashushura,akikagua timu ya mpira wa miguu ya Halmashauri hiyo katika moja ya michezo iliyoandaliwa kwa ajili ya watumishi.
…………..
Na Muhidin Amri, Mbinga
VIJANA Wilayani Mbinga Mkoa wa Ruvuma,wametakiwa kuacha kutazama michezo kama sehemu ya burudani pekee,bali waitumie kama fursa ya kujiajiri,kuimarisha afya na kujenga uchumi wa familia na Taifa.
Wito huo umetolewa jana na Afisa utamaduni na michezo wa Halmashauri ya Wilaya Mbinga Charles Maero,wakati akizungumzia maandalizi ya bonanza kubwa litakalofanyika tarehe 14 mwishoni mwa wiki hii.
Maero alisisitiza kuwa,Serikali imeweka mazingira wezeshi na rafiki ili kuhakikisha vijana wenye vipaji mbalimbali wanatambulika na kuendelezwa ili Taifa liweze kufaidika na vipaji hivyo.
“Michezo ni ajira na uchumi,tunataka kuona vijana wetu wa Mbinga wanatumia nguvu,vipaji na akili zao uwanjani ili kujikwamua kimaisha,huu ni wakati wa kutoka mitaani na kuingia viwanjani”alisema.
Amewataka wananchi wa Halmashauri ya Wilaya na waliopo katika Halmashauri ya Mji Mbinga, kujitokeza kwa wingi kushuhudia bonanza hilo litakalofanyika tarehe 14 Februari 2026 katika uwanja wa CCM Mbinga mjini ikiwa ni sehemu ya kuimarisha mshikamano,umoja, na kuuaga rasmi mwaka 2025.
Maero ametaja michezo itakayochezwa katika bonanza hilo ni mpira wa miguu(soka)mpira wa pete,kukimbia na gunia,kuvuta kamba,riadha na michezo ya asili.
Aliongeza kuwa,timu zote zitakaoshiriki katika bonanza hilo ni Bonde la Hagati na Kigonsera kwa mpira wa miguu na mpira wa pete huku madiwani wa Halmashauri hiyo watachuana na wakuu wa idara na timu zitakazoibuka washindi zitapata zawadi nono.
“Nawaalika wananchi wote wa Mbinga na vitongoji vyake waje kwa wing kushuhudia vipaji kutoka kwa watumishi na madiwani wa Halmashauri ya Wilaya Mbinga,hili sio bonanza la watumishi pekee bali wana Mbinga wote wanaalikwa,waje tushangilie,tufanye mazoezi na kujenga undugu wetu kupitia michezo”alisema Maero.

