‎‎Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Kaspar Mmuya akizungumza na wananchi pamoja na Viongozi mbalimbali waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa nyumba za gharama nafuu kwa wananchi wa kipato cha chini zilizojengwa na Shirika la Habitat for Humanity katika kijiji cha Dabalo kilichopo Wilayani Chamwino Jijini Dodoma tarehe 10 Februari 2026.Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Kaspar Mmuya akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa nyumba za gharama nafuu kwa wananchi wa kipato cha chini zilizojengwa na Shirika la Habitat for Humanity katika kijiji cha Dabalo, Wilaya ya Chamwino Jijini Dodoma, tarehe 10 Februari 2026.

Mwenyekiti wa Bodi ya Habitat for Humanity Tanzania, Bi. Neema Ndikumwami , wa pili kutoka kulia akimkabidhi ufunguo wa nyumba mmoja wa wanufaika wakati wa hafla ya uzinduzi wa nyumba za gharama nafuu zilizojengwa na shirika hilo katika kijiji cha Dabalo, Wilaya ya Chamwino Jijini Dodoma.

Mkurugenzi Mkazi Mkuu wa Habitat For Humanity Tanzania, Bi. Magdalena George, wa pili kutoka kulia akimkabidhi ufunguo wa nyumba mmoja wa wanufaika wakati wa hafla ya uzinduzi wa nyumba za gharama nafuu zilizojengwa na shirika hilo katika kijiji cha Dabalo, Wilaya ya Chamwino Jijini Dodoma.

Na. Meleka Kulwa- Fullshangwe Blog, Dodoma 

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Kaspar Kaspar Mmuya (Mb.) amelipongeza Shirika la Habitat for Humanity Tanzania kwa mchango wake katika kuboresha makazi ya wananchi wenye kipato cha chini, wakati wa hafla ya kukabidhi nyumba 10 za gharama nafuu katika Kata ya Dabalo, Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, ikiwa ni sehemu ya Mradi wa Suluhisho la Makazi Bora na Endelevu (ISSHS).

Ameyasema hayo wakati Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa nyumba za gharama nafuu kwa wananchi wa kipato cha chini zilizojengwa na Shirika la Habitat for Humanity katika kijiji cha Dabalo kilichopo Wilayani Chamwino Jijini Dodoma tarehe 10 Februari 2026

Akizungumza katika hafla hiyo amesema kuwa Serikali inatambua mchango mkubwa unaofanywa na Habitat for Humanity Tanzania katika kuhakikisha wananchi wanapata makazi bora na salama, huku akibainisha kuwa makabidhiano hayo ni sehemu ya nyumba 20 zilizojengwa katika maeneo ya Dabalo Dodoma na Chanika Dar es Salaam.

Aidha amebainisha kuwa shirika hilo limekuwa likitekeleza shughuli zake katika mikoa 13 Tanzania Bara na Zanzibar na kugusa maisha ya Watanzania zaidi ya laki mbili kupitia ujenzi na ukarabati wa nyumba zaidi ya 40,200 pamoja na utoaji wa huduma za maji, usafi wa mazingira na elimu ya haki za ardhi.

Pia ameongeza kuwa ushirikiano uliopo kati ya Habitat for Humanity International na taasisi za kifedha pamoja na Benki Kuu ya Tanzania umewezesha kuanzishwa kwa mikopo ya makazi yenye masharti nafuu kupitia taasisi za fedha ikiwemo NBC na FINCA, hatua inayosaidia wananchi wa kipato cha chini kuboresha makazi yao.

Ameipongeza Habitat for Humanity Tanzania kwa maadhimisho ya miaka 50 kimataifa na miaka 40 hapa nchini tangu mwaka 1986 akisema kuwa mafanikio hayo yanaonesha dhamira ya dhati ya shirika hilo katika kuboresha maisha ya wananchi na kuunga mkono sera za Serikali za ardhi na makazi.

Katika hatua nyingine amesema kuwa matumizi ya teknolojia ya matofali ya kufungana ya udongo yaliyoimarishwa (ISSB) katika ujenzi wa nyumba hizo ni rafiki kwa mazingira na hupunguza gharama za ujenzi huku akibainisha kuwa mradi huo pia umehusisha utoaji wa elimu ya urasimishaji wa ardhi, huduma za maji na matumizi ya nishati jadidifu.

Aidha ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejipanga kuhakikisha kila Mtanzania anapata makazi salama kupitia kurahisisha upatikanaji wa hati miliki, kuongeza uwekezaji katika nyumba za gharama nafuu na kuboresha makazi yasiyo rasmi mijini na vijijini.

Amezitaka taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ardhi ikiwemo NHC, TMRC, TBA, WHC na NCC kushirikiana na Habitat for Humanity katika utekelezaji wa miradi ya makazi kwa wananchi wa kipato cha chini huku akitoa rai kwa sekta binafsi na wafadhili kuunga mkono mpango mkakati wa shirika hilo wa mwaka 2025–2029.

Awali akizungumza kwa Niaba ya Mwenyekiti wa Bodi ya Habitat For Humanity Tanzania, Mkurugenzi wa Miradi wa Habitat for Humanity Tanzania Bw. John Massenza amesema kuwa mradi wa ISSHS unalenga kuboresha hali ya maisha, afya na usalama wa milki ya ardhi kwa kaya zenye kipato cha chini kupitia mbinu bunifu za ujenzi wa nyumba bora na nafuu.

Aidha amebainisha kuwa mradi huo uliotekelezwa kwa mwaka mmoja kuanzia Januari hadi Desemba 2025 umefadhiliwa na Global Mission Fund kwa gharama ya Dola za Kimarekani 199,482.41 sawa na zaidi ya shilingi milioni 509 za Kitanzania, huku akiongeza kuwa wananchi zaidi ya 10,000 wamefikiwa katika maeneo ya Chanika na Dabalo.

Pia ameongeza kuwa katika utekelezaji wake nyumba 20 za mfano zimejengwa, vijana na mafundi zaidi ya 50 wamepatiwa mafunzo ya teknolojia ya ISSB, miti 3,000 imepandwa na mikopo ya ujenzi yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 252 imetolewa kupitia vikundi vya VSLAs kwa kushirikiana na Makazi Bora Finance LTD.

Aidha, amebainisha kuwa ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi, mashirika ya kiraia na wadau wa maendeleo una nafasi kubwa katika kuimarisha upatikanaji wa makazi bora nchini, huku akisisitiza umuhimu wa sera na mipango endelevu itakayowezesha wananchi wa kipato cha chini na cha kati kumudu gharama za nyumba.

Pia, Ameongeza kuwa Habitat for Humanity Tanzania itaendelea kushirikiana kwa karibu na wadau mbalimbali kubuni na kutekeleza miradi jumuishi ya makazi, kutoa elimu kuhusu ujenzi salama pamoja na matumizi bora ya rasilimali ardhi, ili kuhakikisha ndoto ya kila Mtanzania kuwa na makazi yenye hadhi na usalama inatimia.