NA DENIS MLOWE,IRINGA
BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Iringa limekutana leo katika kikao chake cha kawaida, ambapo Meya wa amewataka kuongeza ukusanyaji wa mapato, kuimarisha huduma kwa wananchi, na kusukuma mbele mpango wa kupanua mipaka ya manispaa.
Akizungumza katika ufunguzi wa kikao cha kwanza cha baraza hilo Meya wa Manispaa ya Iringa Ibrahim Ngwada amesisitiza kuwa halmashauri inaendelea kutekeleza wajibu wake wa kisheria wa kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya mikopo sansi kwa vikundi vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.
 Amesema kuwa hatua hiyo inalenga kuinua kiuchumi makundi hayo na kuongeza shughuli za uzalishaji katika manispaa.
Aidha, meya amebainisha kuwa halmashauri inaendelea kutenga asilimia 10 nyingine ya mapato ya ndani kwa ajili ya miradi ya barabara, akieleza kuwa tayari ukarabati kwenye maeneo kadhaa umefanyika katika msimu uliopita ikiwemo barabara ya Kihesa – Kigonzire – Tumaini. Safari hii, halmashauri imeweka lengo la kuongeza kasi ya ujenzi wa barabara za kiwango cha lami kwa kushirikiana na TARURA, kuhakikisha barabara za mjini zinakidhi hadhi ya mji wa utalii kama Iringa.
Meya amesema kuwa kutokana na ongezeko la watalii wanaotembelea Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, ni muhimu barabara za katikati ya mji ziwe za kiwango cha juu ili kuendelea kuvutia wageni na kuongeza mapato ya utalii.
Katika hatua nyingine muhimu, Baraza la Madiwani limejadili mpango wa muda mrefu wa kupanua mipaka ya Manispaa ya Iringa.
Meya Ngwada amesema kuwa halmashauri imeshaanza mchakato huo kwa mujibu wa maagizo ya vikao vya DCC na RCC, ikiwa ni pamoja na kufanya mashauriano na Halmashauri za Iringa Vijijini na Kilolo ili kuandaa mipango ya pamoja kupitia vikao vya kata na vijiji vinavyopendekezwa kuingia ndani ya mipaka mipya ya manispaa.
Amesema malengo ya mpango huo ni kuongeza ukubwa wa eneo la manispaa, kuongeza idadi ya watu, kukuza mapato, pamoja na kuifanya manispaa kuwa katika nafasi nzuri kuelekea hadhi ya Jiji la Iringa katika kipindi kijacho cha miaka mitano.
“Ndani ya miaka hii mitano tunayoenda nayo, tungependa kuona Iringa inakua zaidi ya ilivyo sasa na kuanza safari ya kuwa jiji. Ongezeko la maeneo litatusaidia kupanua huduma, kukuza uchumi na kuongeza hadhi ya mji wetu,” alisema.
Meya ameagiza kuwa mchakato wa upanuzi wa mipaka uanze kutekelezwa mara moja ili kufikia malengo ya muda mfupi na mrefu kwa maendeleo ya wananchi wa Manispaa ya Iringa.