Na Silivia Amandius – Bukoba

Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba, Jacob Nkwera, amesema kuwa mradi wa ujenzi wa kingo za Mto Kanoni unatarajiwa kuanza rasmi tarehe 28 Februari 2026, mara baada ya taratibu zote za kumpata mkandarasi mshauri kukamilika.

Nkwera alitoa kauli hiyo alipokuwa akijibu swali la Diwani wa Kata ya Bilele, Taufiq Sharifu, katika kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika leo Februari 9, katika ukumbi wa Manispaa ya Bukoba. Diwani huyo alitaka kufahamu ni lini mradi huo utaanza kutekelezwa, ikizingatiwa kuwa mkandarasi alishatambulishwa na mkataba kusainiwa zaidi ya miezi sita iliyopita.

Akijibu hoja hiyo, Nkwera alisema hatua ya awali ya kumpata mkandarasi mshauri tayari imekamilika, hivyo kinachosubiriwa ni kuanza kwa utekelezaji wa moja kwa moja wa mradi huo.

“Tumekamilisha hatua ya kumpata mshauri wa mradi, na matarajio yetu ni kwamba kazi zitaanza Februari 28,” alisema Nkwera.

Kwa upande wake, Diwani Taufiq Sharifu alisema wananchi wa maeneo yanayozunguka Mto Kanoni wanaendelea kuishi kwa hofu kubwa kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha na kusababisha mafuriko ya mara kwa mara.

“Tumewaomba kura wananchi na wametuamini, lakini hali inazidi kuwa ngumu. Mvua za siku chache zilizopita zimeshaanza kuleta mafuriko. Wananchi wanateseka na sisi madiwani tunabanwa sana na wananchi wetu. Tunaomba mradi huu uanze mara moja,” alisema Sharifu.

Naye Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Bukoba Mjini, Shabani Mdoe, alisema chama hicho hakiridhishwi na kasi ya utekelezaji wa mradi huo, akisisitiza kuwa kingo za Mto Kanoni ni miongoni mwa miradi muhimu iliyobeba matumaini ya wananchi wa Bukoba Mjini.

Alisema mradi huo ulikuwa sehemu ya ahadi za Ilani ya CCM ya mwaka 2025–2030, na hivyo utekelezaji wake ni wajibu wa serikali.

“Mradi huu unagusa maisha ya wananchi moja kwa moja. Miezi sita ya mkandarasi kukaa kimya ni muda mrefu sana. Tunahitaji utekelezaji uanze haraka ili tuwe na majibu kwa wananchi,” alisema Mdoe.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Erasto Sima, alisema serikali itaendelea kuusimamia mradi huo kwa karibu ili kuhakikisha unaanza kwa wakati, hasa ikizingatiwa kuwa mvua za masika huendelea kuanzia Februari hadi Julai na zimekuwa zikisababisha madhara makubwa kwa wakazi wa maeneo ya kandokando ya mto huo.

Mradi wa ujenzi wa kingo za Mto Kanoni ni sehemu ya miradi ya TACTICS inayotekelezwa katika Manispaa ya Bukoba. Mbali na kudhibiti mafuriko, mkandarasi huyo huyo pia anatarajiwa kujenga barabara kwa kiwango cha lami zenye urefu wa kilomita 10 pamoja na ufungaji wa taa za barabarani.