Habari kwa hisani ya Torch Media

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imethibitisha kuwa utabiri wa mvua za Vuli unaoendelea nchini umeenda sahihi kabisa, baada ya kufikia kiwango cha usahihi cha asilimia 94.1, hatua inayodhihirisha uwezo mkubwa wa kitaalamu wa mamlaka hiyo katika utabiri wa hali ya hewa.

Akizungumza na katika mahijiano jijini Dar es Salaam yaliyofanyika ofisini kwake jijini Dar es Salaam, Mtaalamu wa Hali ya Hewa kutoka TMA, Alfred Kondoya, amesema mwenendo wa mvua pamoja na hali ya hewa uliojionesha katika maeneo mbalimbali nchini umeendana kwa kiwango kikubwa na makadirio ya awali yaliyotolewa na TMA.

Amesema kiasi cha mvua kilichonyesha pamoja na mwelekeo wake katika maeneo tofauti kimekuwa kikilingana na takwimu na asilimia za utabiri uliotolewa, hali inayoonesha usahihi mkubwa wa data na mifumo ya kisasa ya utabiri inayotumiwa na mamlaka hiyo.

Hata hivyo, Kondoya amebainisha kuwa licha ya usahihi huo, mvua za Vuli zimekuwa na mtawanyiko usio wa kawaida katika baadhi ya maeneo, jambo lililosababisha changamoto kwa shughuli za kilimo, hususan kwa wakulima waliotegemea ratiba maalumu ya msimu wa upandaji.

Kutokana na hali hiyo, TMA imeendelea kuwataka wananchi na wadau mbalimbali kufuatilia kwa karibu taarifa za hali ya hewa zinazotolewa mara kwa mara ili kuchukua tahadhari mapema na kupanga shughuli zao kwa ufanisi zaidi.

Wakati huohuo, TMA imetangaza kuwa inatarajia kutoa rasmi utabiri wa mvua za Masika mwanzoni mwa mwezi Februari mwaka huu, utabiri utakaohusu kipindi cha kuanzia Machi hadi Mei.

Kondoya amesema utabiri huo ni muhimu kwa mipango ya sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, maji, nishati na miundombinu, hivyo amewataka wananchi kuwa wavumilivu na kusubiri tangazo rasmi ili kupata mwelekeo sahihi wa msimu wa Masika.

Ameongeza kuwa kabla ya kutolewa kwa utabiri huo, TMA imekuwa ikifanya vikao vya mashauriano na taasisi mbalimbali za Serikali na wadau ikiwemo DAWASA, Wizara ya Maji, Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na taasisi nyingine, kwa lengo la kubaini changamoto na kutoa ushauri wa kitaalamu kulingana na mahitaji ya maeneo husika.