Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA ,Injinia Wolta Kirita akisaini makubaliano hayo katika Chuo cha ufundi (ATC) Arusha leo.

Mkuu wa chuo cha ufundi Arusha ,Profesa Mussa Chacha akizungumzia mara baada ya kusaini makubaliano hayo .

………..
Na Happy Lazaro, Arusha
Chuo cha ufundi Arusha (ATC) kimesaini hati ya makubaliano na Ruwasa kuhusu uzalishaji wa mita janja ambazo zinaruhusu malipo kabla ya matumizi ya huduma za maji ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya Rais.
Akizungumza mara baada ya kusaini hati hiyo Mkuu wa chuo cha ufundi Arusha ,Profesa Mussa Chacha amesema kuwa , chuo cha ufundi Arusha kina majukumu matatu ikiwemo kufundisha ,kufanya utafiti na kutoa ushauri wa kitaalamu ambapo hili eneo la utafiti ndilo hasa limewafanya kuwa na mahusiano na Ruwasa .
Amesema kuwa ,Ruwasa walikuwa na changamoto ya kiutendaji ambapo walitaka wananchi wapate mita janja (smart Meter ) ambapo waliingia makubaliano ya kuanza kufanya utafiti wa miaka mitatu kwa pamoja ambapo mwishoni waliweza kupata mita ambazo zinafaa na zilizoboreshwa .
Ameongeza kuwa, tayari wananchi wana uelewa kuhusu mita hizo na kuna wananchi ambao tayari wanazitumia ambapo wamegundua kuwa zinafanya kazi vizuri kwa mazingira ya kitanzania na ndio maana leo wakafikia hatua ya kuingia makubaliano na Ruwasa kwa ajili ya kuanza uzalishaji wa hizo mita kwa wingi .
“Sisi chuo cha ufundi Arusha tunawahakikishia Ruwasa kuwa Teknolojia tunayo na wameshaidhibitisha na uwezo wa kuzalisha pia tunao na ukiangalia chuo cha ufundi Arusha tuna wanafunzi zaidi ya 5,000 hapo chuoni hivyo kiwanda hicho licha ya kwamba kinatumika kwenye uzalishaji bali ni sehemu ya mafunzo kwa wanafunzi wao ambapo hata wataalamu wanaojua teknolojia hiyo watawaajiri baadaye .”amesema Prof Chacha .
Ameongeza kuwa ,mita hizo zinatengenezwa na watanzania kwa maana ya wataalamu wa ndani ambao pia wametengeneza mfumo mzima wa hizo mita ambapo hata matengenezo yale wataalamu wa ndani ndo watakuwa wanafanya na zoezi hili ni endelevu .
“Kupitia hizi mita tutaweza kuharakisha maendeleo ya watanzania kwani wanaotengeneza ni watanzania na vijana watapata ajira kupitia uzalishaji huo kwani mchakato huo umekuwa ni jumuishi na utasukuma maendeleo ya watanzania.”amesema Profesa Chacha .
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA ,Injinia Wolta Kirita amesema kuwa uwekaji wa mita ni sehemu ya uwekezaji ambapo mita hizo zitafungwa kwa gharama za Ruwasa na kwa zile gharama ambazo wananchi wamechangia katika ununuzi wa maji .
Injinia Kirita ameongeza kuwa,baada ya makubaliano hayo kinachofuata sasa hivi ni kutoa elimu ambapo watakutana na mameneja wa mikoa,wilaya ,na watatoa elimu ambapo watakuwa wanashirikiana na chuo hicho kwani kuna maswali ambayyo wananchi wanaweza wakaja nayo hivyo ni vizuri wakashirikiana na chuo hicho kutoa elimu ili wananchi waelewe umuhimu wa hizo mita jinsi zinafanya kazi.




