Na Hellen Mtereko,Mwanza
Mabaunsa watatu wanaodaiwa kukodiwa na Mwekezaji wa Kampuni ya LEWICO ya Jijini Mwanza, wamezua tafrani iliyodumu kwa zaidi ya saa tatu baada ya kufunga chumba cha duka la Mjane wa Marehemu Michael Misigaro katika eneo la maduka ya Shule ya Sekondari Pamba jijini humo.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya taharuki hiyo Adelina Mkina, ambaye ni mmiliki wa duka hilo Na.TK2, amesema alikuta mabaunsa watatu wakiwa tayari wamefunga chumba cha duka lake alilomilikishwa kihalali na Halmashauri ya Jiji la Mwanza kwa maelekezo ya Wilson Tarimo ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya LEWICO, anayedai kwamba ndiye mwekezaji wa maduka hayo.
“Mimi ni mjane na ninawatoto watano sasa anavyokuwa ananitishia kufunga biashara yangu anataka watoto wangu wahudumiwe na nani,mimi natakiwa kulipa Kodi Jiji na siyo kwake naomba sana Serikali mnisaidie naumia sana”, ameeleza Adelina
Novemba 20, 2024 Adelina Mkina alikubaliwa na Halmashauri ya Jiji la Mwanza kuwa mpangaji kupitia zabuni ya marudio ya upangishaji wa maeneo mbalimbali ya biashara.
Akizungumza kwa njia ya simu Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba amesema anamtambua Adelina kama mpangaji halali kuanzia Julai 01, 2024.
“Sisi tunamtambua huyo mama hata akienda mahakamani tutakuwa mashahidi wake kwasababu tunamkataba naye”, alieleza Kibamba
