Msitu wa Pugu Kazimzumbwi, hazina ya asili iliyopo karibu na Jiji la Dar es Salaam, umeendelea kuwa kivutio kikubwa cha utalii wa ikolojia kwa wananchi wanaotafuta mapumziko, burudani na uzoefu wa kipekee wa kuishi karibu na mazingira ya asili, hususan katika msimu huu wa sikukuu.
Hifadhi hiyo inajivunia vivutio mbalimbali vya kipekee vikiwemo viumbe hai, mimea ya asili, matembezi ya msituni (nature walks) pamoja na fursa ya kulala kwenye mahema (tenti), ambavyo vimeendelea kuwavutia watalii wa ndani wanaopenda utalii wa mazingira.
Miongoni mwa watalii waliotembelea hifadhi hiyo ni Sclora Mwasenga, ambaye amesema yeye na wenzake wamefurahishwa na kile walichokishuhudia, akieleza kuwa Pugu Kazimzumbwi ni eneo lenye utajiri mkubwa wa vivutio vya aina mbalimbali vya utalii.
“Tumefurahi sana kufika hapa. Tumeona utalii wa kila aina unaopatikana katika eneo hili, kuanzia viumbe hai, mimea ya asili hadi shughuli mbalimbali za ikolojia. Ni sehemu ambayo Watanzania wengi wanapaswa kuitembelea,” amesema Mwasenga.
Ameongeza kuwa uamuzi wao wa kufika katika hifadhi hiyo ulitokana na kuona picha na taarifa zilizochapishwa kupitia mitandao ya kijamii ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), hali iliyowahamasisha kujionea vivutio hivyo kwa macho yao.
Kwa upande wake, Vellonica, mmoja wa watalii, amesema safari yao imekuwa ya kufurahisha kwa kiwango kikubwa, hasa kutokana na kupata uzoefu wa kipekee wa kulala kwenye tenti katikati ya mazingira ya asili.
“Tumeenjoy sana. Awali hatujawahi kupata uzoefu wa kulala kwenye tenti msituni. Ni jambo la kipekee na la kuvutia sana,” amesema.
Hifadhi ya Msitu wa Pugu Kazimzumbwi ina vivutio vingi vya utalii wa ikolojia ikiwemo kutazama viumbe hai mbalimbali, kujifunza kuhusu mimea ya asili, utalii wa mitumbwi katika maeneo maalum, pamoja na matembezi ya asili kupitia njia salama zilizopo ndani ya msitu. Kupitia shughuli hizo, watalii hupata fursa ya kufurahia mandhari ya asili, hewa safi na utulivu wa mazingira.
Naye Regina Mwakifuna, Mhifadhi Msaidizi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), ametoa wito kwa Watanzania kujitokeza kwa wingi kutembelea msitu huo, hususan katika msimu huu wa sikukuu.
“Tunawakaribisha Watanzania wote kufika Pugu Kazimzumbwi. Ni eneo zuri, salama na linafaa kwa makundi yote, ikiwemo kina mama wanaotaka ‘kuvunja vikoba’ kwa kupumzika na kufurahia mazingira ya asili,” amesema Mwakifuna.
Msitu wa Pugu Kazimzumbwi unaendelea kuwa mfano bora wa namna uhifadhi wa rasilimali za asili unavyoweza kuchangia maendeleo ya utalii wa ndani na ustawi wa jamii kwa ujumla.

