
Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ilala, chini ya uongozi wa Mwenyekiti Comrade Mohamed Msophe, imetembelea nyumbani kwa familia ya marehemu Abdulswamad Abdulazizi Abdulswamad, aliyekuwa Katibu wa Jumuiya hiyo katika Kata ya Mchafukoge, kwa lengo la kuwafariji na kutoa pole.
Akizungumza na familia ya marehemu leo, Desemba 18, 2025, jijini Dar es Salaam, Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Ilala, Comrade Mtiti Jirabi Mbassa, ametoa salamu za rambirambi kwa niaba ya Jumuiya hiyo. Huku akiwasihi wanafamilia kuwa na moyo wa uvumilivu katika kipindi hiki kigumu na kuendelea kumuombea marehemu kwa Mwenyezi Mungu.
Comrade Mbassa ameeleza kuwa marehemu alikuwa mtumishi mwadilifu na mchapakazi aliyetekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa, hivyo Jumuiya imepata pigo kubwa kwa kumpoteza kiongozi muhimu.
Kwa upande wao, baadhi ya wajumbe wa Baraza la Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Ilala waliokuwepo wamesisitiza umuhimu wa kuenzi na kuiga mema ya marehemu, huku wakitoa maneno ya faraja na matumaini kwa watoto wa marehemu.
Nao viongozi wa Jumuiya ya Wazazi, akiwemo Katibu wa Jumuiya hiyo Mkoa wa Dar es Salaam, Comrade Haji Kilimo, ametuma salamu za rambirambi kwa niaba ya uongozi wa mkoa.
Marehemu Abdulswamad Abdulazizi Abdulswamad alifariki dunia Desemba 4, 2025, na kuzikwa Desemba 5, 2025 katika Makaburi ya Kisutu, jijini Dar es Salaam.
