Na.Sophia Kingimali.
Msemaji Mkuu wa Serikali na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, amewataka waandishi wa habari za mitandaoni kutumia kalamu zao kujenga taifa badala ya kubomoa huku akisisitiza kuwa waandishi wa habari ni wadau muhimu katika kulinda amani, mshikamano na maendeleo ya Tanzania.
Hayo amlleyasema leo Disemba 18 katika kikao kazi kati ya waandishi wa habari za mtandaoni na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA Msigwa amesema kuwa tangu alipoteuliwa kushika nyadhifa mbalimbali serikalini, ikiwemo Idara ya Habari na sasa kuwa Msemaji Mkuu wa Serikali, amekuwa na dhamira ya kushirikiana na waandishi wa habari kwa misingi ya kuaminiana, akibainisha kuwa imani huzaa imani kati ya serikali na wanahabari.
“Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa maelekezo ya wazi ya kuwawezesha waandishi wa habari, hususan wa mitandaoni, ili wafanye kazi zao katika mazingira salama, huru na yenye kuzingatia taaluma”,Amesema Msigwa.
Ameongeza kuwa wizara husika kwa kushirikiana na taasisi kama TCRA zinatekeleza maelekezo ya Rais kwa kufanyia kazi changamoto za kisheria, kanuni na sera zinazowakabili waandishi wa habari, akisisitiza kuwa serikali iko tayari kurekebisha sheria, kanuni au sera zitakazoonekana kikwazo katika utekelezaji.
Amesisitiza kuwa Tanzania ni nchi salama kwa waandishi wa habari kufanya kazi zao na kwamba waandishi wa habari wana haki ya msingi ya kufanya kazi ndani ya nchi yao bila hofu, huku serikali ikiahidi kusikiliza hoja zao na kuzitatua kwa maslahi mapana ya taifa.
Akizungumzia suala la leseni na kodi, Msigwa amesema kuwa utaratibu wa leseni ni muhimu katika kulinda taaluma ya uandishi wa habari, ili kuepusha kila mtu asiye na sifa kujitambulisha kama mwandishi wa habari, jambo linaloweza kuharibu taswira ya taaluma hiyo.
Aidha, ameeleza kuwa serikali inatambua mchango mkubwa wa waandishi wa habari za mitandaoni katika kukuza uchumi kupitia kuhamasisha uwekezaji, utalii na ulipaji kodi, akisisitiza kuwa habari chanya zinaweza kuingizia taifa mapato makubwa zaidi kuliko gharama za uendeshaji wa sekta hiyo.
Msigwa ameonya dhidi ya matumizi mabaya ya majukwaa ya mitandaoni yanayoendeshwa kwa maslahi binafsi au kutoka nje ya nchi, akisema yapo majukwaa yanayotumika kupotosha taarifa na kuharibu taswira ya Tanzania kama nchi ya amani, utulivu na mshikamano.
Kwa kumalizia, Msemaji Mkuu wa Serikali ameahidi kuwa serikali iko katika mchakato wa kuanzisha Mfuko wa Waandishi wa Habari utakaowezesha wanahabari kupata mikopo na vitendea kazi, huku akiwataka waandishi wa habari za mitandaoni kuwa mstari wa mbele kulinda maslahi ya taifa na kuhakikisha simulizi njema ya Tanzania inaendelea kusikika ndani na nje ya nchi.

