Wakulima nchini wametakiwa kuongeza matumizi ya teknolojia ya kilimo mahiri ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, kwa kulima mazao yanayohimili ukame kama mikunde, mtama na mihogo.
Akizungumza mjini Morogoro pembezoni mwa mkutano uliowakutanisha wadau wa utekelezaji wa sera za kilimo na mazingira, Mkuu wa Idara ya Kilimo, Uchumi na Biashara wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dkt. Innocensia John, alisema mazao ya asili yana uwezo mkubwa wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi na kuongeza tija kwa wakulima.
“Endapo wakulima wataendelea kupanda mazao ya asili yenye uwezo wa kustahimili ukame, watakuwa na uhakika wa chakula na pia watazalisha mazao mengi katika eneo dogo. Hii ndiyo njia sahihi ya kujenga ustahimilivu kwenye kilimo,” alisema Dkt. Innocensia John.
Naye Dkt. Aloyce Hepelwa, Msimamizi wa Mradi wa Uchumi Jumuishi wa Kijani (IGE) wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema mradi huo wa miaka minne utakaokamilika mwaka 2027 unalenga kuleta matokeo chanya katika sekta ya kilimo na mazingira.
“Mradi wa IGE umejikita katika kuwezesha jamii kutumia rasilimali kwa tija bila kuathiri mazingira. Tunatarajia kuona ongezeko la uzalishaji, uhifadhi wa mazingira na matumizi endelevu ya ardhi ifikapo mwisho wa mradi,” alisema Dkt. Aloyce Hepelwa.
Kwa upande wake, Bwana Vedastus Sitta, Meneja kutoka Tume ya Taifa ya Mipango, alipongeza hatua ya wadau kujadili kwa kina kuhusu Kilimo Mahiri (Climate Smart Agriculture), akibainisha kuwa kilimo hicho kimetajwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
“Dira ya Taifa ya 2050 imeelekeza kuwa miradi yote inayotekelezwa nchini izingatie utunzaji wa mazingira. Kilimo mahiri ni sehemu muhimu ya kufikia uchumi shindanishi na unaostahimili mabadiliko ya tabianchi,” alisema Bwana Vedastus Sitta.
Mkutano huo umeendelea kutoa mapendekezo ya kitaalamu kuhusu namna bora ya kuimarisha kilimo nchini huku wakulima wakihimizwa kukumbatia teknolojia na mbinu za kisasa ili kuongeza ustahimilivu na uzalishaji.

