Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Mwenyekiti wa Biashara wa Jumuiya ya Madola na Baraza la Uwekezaji (CWEIC), Lord Hugo Swire, leo tarehe 02 Desemba, 2025, Ikulu jijini Dar es Salaam.

Katika mazungumzo hayo, viongozi hao wamejadili fursa za ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji, zikiwemo juhudi za kuvutia mitaji na kukuza ajira kwa Watanzania.

Taarifa iliyotolewa na Shaaban Kissu Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais – Ikulu imesema Rais Dkt. Samia amesema Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na kuimarisha mifumo ya kiutendaji ili kuwahakikishia wawekezaji usalama wa mitaji yao pamoja na ustawi wa biashara. Amesisitiza kuwa Tanzania imejenga misingi imara ya ushirikiano wa maendeleo kwa zaidi ya miongo sita, hatua inayoweka mazingira mazuri ya ushiriki wa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Aidha, akirejea tukio la uvunjifu wa amani la tarehe 29 Oktoba, 2025, Mhe. Rais amebainisha kuwa Tanzania inabaki kuwa taifa lenye utulivu na mfumo madhubuti wa kusimamia masuala ya usalama wa raia na mali zao. Amesema Serikali itaendelea kuchukua hatua stahiki kuhakikisha amani, utulivu wa biashara na miundombinu ya uwekezaji vinaimarika.

Vilevile, ameeleza kuwa Tanzania ipo katika hatua za awali za mchakato wa mapitio ya Katiba, hatua ambayo inalenga kuimarisha taasisi, mifumo ya haki za kiuchumi, sekta binafsi na uwekezaji.

Kwa upande wake, Lord Swire amepongeza juhudi za Serikali katika kuimarisha uchumi na mazingira ya uwekezaji, huku akieleza dhamira ya CWEIC kuendelea kushirikiana na Tanzania kama mshirika wa kimkakati wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola.

Ameshukuru kwa mapokezi aliyoyapata Ikulu na ameahidi kushirikiana na Tanzania katika kuvutia wawekezaji wapya kutoka mataifa wanachama, sambamba na kuiombea nchi iendelee kuwa yenye utulivu na amani.